Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatma ya Yemeni iko kwenye Kongamano la Maridhiano lijalo:UM

Hatma ya Yemeni iko kwenye Kongamano la Maridhiano lijalo:UM

Kongamano kwa ajili ya kujadilia mustakabala wa kisiasa wa taifa la Yemen lililopangwa kufanyika mwaka ujao, linaweza kuwa ndiyo mwarubaini kwa kuikwamua nchi hiyo ambayo kwa sasa ipo katika kipindi cha mpito lakini ikiandamwa na mchanganyiko wa mikwamo mbalimbali.

Hayo ni kwa mujibu wa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa taifa hilo Jamal Benomar ambaye amesema kuwa hali jumla kwa taifa hilo bado ni tete.

Akitoa taarifa yake mbele ya Baraza la Usalama, mjumbe huyo ameeleza kuwa mustakabala jumla wa taifa hilo sasa unasalia mikononi mwa kongamano hilo na kama litafaulu basi enzi mpya ya mafungamano ya kweli itazaliwa na kama litashindwa basi kunatazamiwa kujitokeza kwa mkwamo wa pekee.

Makundi yanayohasimiana yaliingia kwenye makubaliano mwezi Novemba mwaka jana 2011 yakikubali kupisha kipindi cha mpito na kuanzisha duru mpya ya majadiliano ili hatimaye kufikia suluhu ya kudumu.