Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani vikali mashambulizi katika mji wa Kano, Nigeria

Ban alaani vikali mashambulizi katika mji wa Kano, Nigeria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali muendelezo ya matukio ya mashambulizi nchini Nigeria na kuyaita mashambulizi ya hivi karibuni katika mji wa Kano yaliyosababisha mamia ya watu kupoteza maisha kuwa ni tukio la kinyama na lisilovumilika.

Zaidi ya watu 150 wamepoteza maisha na mamia wengine kujeruhiwa vibaya kufuatia shambulizi hilo ambalo linadaiwa kufanywa na waafuasi wa kundi la Bokoharam ambalo linamafungamano na kundi la Taliban la nchini Afghanistan.

Ikiwa ni mfulululizo wa mashambulizi yanayoendelea kuindamaa Nigeria, shambulizi  hilo la mwisho wa juma, lililenga majengo ya polisi pamoja na ofisi za uhamiaji.

Katika taarifa yake kulaani matukio hayo, Ban amesema kuwa ameshtushwa na kusikitishwa na mwenendo wa matukio hayo ambayo amesema hayapaswi kuungwa mkono kwa jinsi yoyote ile.

Amewatia moyo wananchi wa Nigeria na serikali yao akisema huu ni wakati wa kushikamana na ametaka kufanyika uchunguzi ili wahusika wake waletwe kwenye mkono wa sheria.