Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNESCO asisitiza haja ya ubunifu kuhakikisha hadhi na elimu bora

Mkuu wa UNESCO asisitiza haja ya ubunifu kuhakikisha hadhi na elimu bora

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO leo amesisitiza ukweli kwamba taarifa na teknolojia ya mawasiliano vinaweza kutumika kuhakikisha kuna elimu bora na fursa sawa za kusoma hata katika nchi ambazo ziko nyuma kwa sababu ya ukosefu wa rasilimali. Bi Irina Bokova akizungumza katika mkutano wa kimataifa wa mawaziri wa elimu unaoendelea mjini London amesema kupiga hatua ni zaidi ya suala la fedha, ni suala la kukidhi mahitaji.

Akifafanua kwamba ni kuwa wabunifu katika teknolojia, ni kujenga ubunifu huo na sekta binafsi kama kupitia muungano wa kimataifa wa washirika wa elimu ambao utaanzishwa mwaka huu wenye kauli mbiu ya kujifunza kutokana na mabadiliko muhimu duniani.

Ameongeza kuwa kuna haja ya kuifanya elimu kuwa nguvu ya kuleta mageuzi kwa heshima ya binadamu, pia katika masuala ya kijamii, kiuchumi na mabadiliko ya kisiasa. Amesema kizazi kipya kinahitaji elimu ambayo itawapa ujuzi na kutumia teknolojia katika soko la kazi.