Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon amezingatia, kwa wasiwasi mkubwa, uamuzi wa karibuni wa Serikali ya Isarel wa kuidhinisha ujenzi ziada wa majumba ya walowezi kwenye Maeneo Yaliokaliwa Kimabavu ya WaFalastina. Vitendo hivi na makazi yote ya walowezi kwenye maeneo yaliokaliwa, alisema KM ni vitendo vinavyoharamisha sheria ya kimataifa na ile Ramani ya Mpango wa Amani. KM ameisihi Israel kuzingatia juhudi muhimu za kuandaa mazingira ya kuridhisha ya majadiliano ya amani kati ya WaFalastina na Waisraili, yenye uzito unaoaminika na wote. KM alirudia tena ule mwito unaoitaka Israel kusimamisha shughuli zote za maeneo ya ulowezi, ikijumlisha ujenzi unaodaiwa kuwa wa kimaumbile, na kuitaka Israel vile vile kung\'oa vituo vyote vya ukaguzi vilivyojengwa kwenye maeneo yaliokaliwa ya WaFalastina tangu mwezi Machi 2001.

Baraza la Usalama asubuhi lilizingatia suala juu ya Shirika la Ulinzi Amani katika Liberia (UNMIL). Ellen Löj, Mjumbe Maalumu wa UM kwa Liberia alielezea maendeleo kuhusu ujenzi wa amani na utulivu katika Liberia. Kadhalika, Baraza lilisikiliza ripoti kutoka Balozi wa Ujapani, Yukio Takasu aliye mkuu wa Kamati ya Vikwazo dhidi ya Iran, juu ya namna mataifa wanachama yanavyotekeleza maazimio ya Baraza la Usalama juu ya Iran. Halkadhalika, alasiri Baraza la Usalama lilizingatia Haiti ambapo Mjumbe Maalumu wa UM kwa Haiti, Raisi Mstaafu wa Marekani Bill Clinton pamoja na Mjumbe Maalumu wa KM kwa Haiti, Hédi Annabi walihutubia na kuzingatia maendeleo kwenye utekelezaji wa mpango wa amani nchini Haiti.

Kai Eide, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afghanistan, ametoa taarifa yenye kuelezea huzuni kuu aliyopata kufuatia taarifa za kifo cha mwandishi habari mzalendo Sultan Munadi, ambaye aliuawa baada ya kufanyika operesheni ya ukombozi kutoka kizuizini waliposhikwa na kundi la Taliban. Mwandishi habari mwengine aliyekuwa naye kizuizini humo, Stephen Farrell wa gazeti la Marekani la New York Times, aliokolewa salama na vikosi vya kimataifa. Eide alikumbusha juu ya hatari ya maisha wanaokabiliwa nayo kila siku waandishi habari wanaofanya kazi katika Afghanistan. Aliwasihi watawala wa kienyeji na makundi yanayowapinga wenye mamlaka Afghanistan, kuhishimu haki za waandishi habari kuendeleza kazi zao kwa usalama na bila ya hatari ya kuangamizwa au kutekwa nyara.

Sha Zukang, Naibu KM juu ya Masuala ya Uchumi na Jamii anahudhuria hivi sasa Mkutano wa 2009 wa Kuimarisha Mazingira katika Korea, unaofanyika kwenye mji mkuu wa Seoul, Jamhuri ya Korea (Korea ya Kusini). Mkutano unasailia taratibu za kuimarisha ushirikiano bora baina ya serikali na viwanda, kwa makusudio ya kupunguza na kudhibiti bora athari za hewa chafu unayomwagwa angani. Kwenye risala yake mkutanoni, Sha alielezea umuhimu wa kuyasaidia mataifa yanayoendelea kushirikishwa kidhati kwenye harakati za kile alichokiita "mapinduzi ya viwanda vitakavyotunza mazingira kijani".