Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon wiki ijayo atafanya ziara ya siku mbili katika Svalbard, Norway, ili kujionea binafsi athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika eneo la Kaskazini ya dunia la Akitiki (Arctic). Kwanza KM atakwenda eneo la Ny-Alesund, liliopo Kaskazini kwenye fungu la visiwa vya Svalbard, ambapo atazuru steshini ya uchunguzi juu ya mazingira ya ncha ya dunia, kabla hajaelekea Kaskazini juu zaidi ambapo atapatiwa taarifa mpya za kisayansi kuhusu namna majabali ya barafu yanavyodhibiti na kurekibisha shughuli za Bahari ya Akitiki na kuathiri mabadiliko ya hali ya hewa ya ulimwengu.

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti hali katika mji wa Sa'ada, Yemen kaskazini ni ya kutia wasiwasi mkuu, wakati mapigano yanaendelea katika eneo ambalo limetengwa kabisa kutoka sehemu nyengine za nchi kwa karibu wiki moja sasa. Kamishna Mkuu wa UM juu ya Wahamiaji, Antonio Guterres, amependekeza kufunguliwe ujia maalumu Yemen kaskazini, utakaowaruhusu raia kuhamishwa kutoka eneo la mapigano na kuwawezesha wahudumia misaada ya kiutu kuendeleza operesheni za kukidhi mahitaji ya kimsingi kwa maelfu ya raia waliong'olewa makazi, hasa ilivyokuwa serekali imetangaza hali ya dharura kwenye sehemu hii ya nchi, na raia hawaruhusiwi kuondoka makwao. Hivi sasa watu wingi wanamudu maisha kwa kufadhiliwa misaada na marafiki pamoja na jamaa waliobahatika kuwa na akiba ya chakula.

Baraza la Usalama, kwa kuitika ombi la Serikali ya Lebanon, Alkhamisi lilipitisha, bila ya kupingwa, azimio la kuongeza muda wa operesheni za Vikosi vya UM vya Uangalizi wa Kusitisha Mapigano Lebanon (UNIFIL), mpaka 31 Agosti 2010. Kadhalika, imeripotiwa Ijumaa asubuhi vikosi vya UNIFIL viliwakabidhi wenye mamlaka wa Israel raia wao mmoja ambaye aliashiriwa kuwa ni mgonjwa wa akili. Iliripotiwa mtu huyo Ijumanne alivuka mpaka na kuingia Lebanon kutoka Israel kwenye eneo linalojulikana kama Msitari wa Buluu. Mgonjwa huyo alikabidhiwa wahusika kwa kulingana na maafikiano yao na UNIFIL.

Ray Chambers, Mjumbe Maalumu wa KM juuya Udhibiti Malaria karibuni alizuru Tanzania na Uganda kutathminia hali halisi ilivyo katika utekelezaji wa miradi kinga dhidi ya malaria. Kwenye ripoti yake aliowakilisha kwa Ban Ki-moon alisema ana imani kuwa utafanikiwa kulifikia lengo la KM la kuhakikisha mataifa yote yenye kuhitajia msaada wa kudhibiti maradhi hayo yatapatiwa uwezo huo katika 2010. Chambers alisema asilimia 52 ya zile sehemu za Afrika kusini ya Sahara, zenye kusumbuliwa na malaria zimefanikiwa kupatiwa vyandarua vilivyonyunyiziwa dawa za kuua vijidudu vinavyosababisha malaria.

Msemaji wa KM ametangaza taarifa ya kusahihisha ripoti ya Ijumatatu juu ya kifo cha Shyamlal Rajapaksa, mwendesha mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR). Kwa mujibu wa taarifa zilizopokewa kutoka msemaji wa ICTR, Roland Amoussouga, uchunguzi wao umethibitisha Rajapaksa alifariki kwa sababu ya ugonjwa na sio kitendo cha uhalifu dhidi yake. Upelelezi wa polisi vile vile umethibitisha kwamba hakuna ushahidi kama kulifanyika kosa la kuua. Sababu hasa za kifo bado hazijatambuliwa na ICTR inasubiri ripoti ya uchunguzi wa taaluma ya sumu kutoka maabara kutambua kiini halisi cha kifo cha mtumishi huyo wa ICTR.