Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Wajumbe wa Baraza la Usalama walikutana kwenye kikao maalumu cha faragha, hii leo, kusikiliza ripoti ya Mike Smith, mkuu wa Kurugenzi ya Utendaji Dhidi ya Ugaidi, ambapo pia walisailia shughuli za miezi ya karibuni ya bodi hilo.

Kwenye mkutano, wa kila mwezi na waandishi habari waliopo Makao Makuu ya UM, uliofanyika adhuhuri ya leo mjini New York, KM Ban Ki-moon aliihadharisha jumuiya ya kimataifa kutoingiwa kihoro kisio na msingi, au kupatwa na wasiwasi kwasababu ya tangazao la Shirika la Afya Duniani (WHO) la kupandisha juu kiwango cha tahadhari ya maambukizi ya virusi vipya vya homa ya mafua ya A(H1N1), kutoka daraja ya 5 hadi 6. Alitilia mkazo kwamba walimwengu wanawajibika sasa hivi kujitayarisha, kwa kila njia, kukabiliana na mripuko wa maambukizi ya maradhi haya. KM aliwaambia waandishi habari hatua iliochukuliwa na WHO, ya kupandisha juu daraja ya maambukizo, ni kitendo "kilichothibitisha rasmi juu ya kuenea kijografia kwa ugonjwa huo" na haimaanishi umekusudiwa "kuchochea khofu na wasiwasi kwa umma wa kimataifa." Alisema licha ya kuwa homa ya mafua ya H1N1 ni ugonjwa wa kuambukiza, kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa wataalamu wa afya, virusi vyake havikuonyesha ukali wa kudhuru wanadamu, kama ilivyokhofiwa hapo kabla, hasa ilivyokuwa kima cha vifo vilivyosababishwa na virusi vipya vya H1N1 ni kidogo. Hata hivyo, KM aliitaka jamii ya kimataifa kuendelea kuwa "waangalifu" kwa sababu hakuna ajuaye ni sura gani maradhi haya yatachukua mnamo miezi ijayo. Alikumbusha KM kwamba virusi vya homa ya H1N1, kwa sasa, vimesambaa zaidi kwenye nchi zilizoendelea .. na hali hiyo inabashiriwa huenda ikabadilika haraka - na kuzusha taathira kadha wa kadha kimataifa. Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dktr Margaret Chan, yeye kwa upande, wake alithibitishia rasmi, kutoka Geneva, ya kuwa ulimwengu sasa hivi "umeingia kwenye mkondo wa awali wa 2009, uliovamiwa na janga la ugonjwa wa homa ya mafua ya H1N1" ambapo, kwa mujibu wa takwimu rasmi za UM leo hii watu "30,000 katika nchi 74 walishasajiliwa kuambukizwa na maradhi hayo."

Vile vile kwenye mahojiano hayo ya Alkhamisi na waandishi habari katika Makao Makuu KM Ban Ki-moon alizungumzia masuala mengine yanayohusu matatizo ya uchumi duniani, ambapo alionya yasitumiwe na Mataifa Wanachama matajiri kama ni kisingizio cha kukwepa kutekeleza ahadi walizotoa kwenye mkutano uliofanyika Gleneagles, Scotland mwaka 2005, za kuzisaidia nchi za Afrika kuhudumia maendeleo. Alizungumzia pia juu ya masuala yanayohusu usalama na amani katika Mashariki ya Kati, na kutilia mkazo kwamba WaFalastina na Waisraili wana haki ya kujiamulia wenyewe, na haki ya utaifa na usalama. Kadhalika KM alipongeza uchaguzi wa Lebanon uliofanyika majuzi, ambao alisema uliendelezwa kwa amani na bila fujo. Halkadhalika, KM aligusia masuala kuhusu majukumu yalioikabili Serikali ya Sri Lanka katika kurudisha utulivu nchini, kwa kulingana na ahadi alizopewa wakati alipozuru eneo hilo karibuni. Wakati huo huo aliihimiza Serikali ya Sri Lanka kuwajumuisha kwenye shughuli za kizalendo, za utawala, wale raia walio wachache wenye asili ya KiTamili, ikiwa wenye mamlaka wamedhamiria kujiepusha na madhara ya kihistoria ya kuzusha vurugu kwa sababu ya kuwatenga raia hao. Kuhusu hali ya Pakistan, KM alisema ilimtia wasiwasi mkubwa, hususan lile shambulio la karibuni la katika mji wa Peshawar, ambapo WaPakistani kadha waliuawa pamoja na watumishi wawili wa UM kutoka Serbia na Phillipones, na pia wafanyakazi watatu wengine wa UM, raia wa Pakistan.

Asubuhi, Baraza la Usalama lilikutana kwenye kikao cha hadhara kusikiliza ripoti ya John Holmes, Mratibu wa Misaada ya Dharura ya UM na Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu kuhusu ziara yake ya Aprili Sudan kufuatia kufukuzwa nchini humo mashirika kadha ya kigeni yaliokuwa yakihudumia misaada ya kiutu. Alisema kufukuzwa kwa jumuiya hizi za kiraia kulikuwa ni makosa na ni kitendo kisioweza kutetewa, hali ambayo alisema ilisababisha maisha hatari kwa mamia elfu ya raia wa Darfur waliokuwa wakitegemea misaada. Alisema mashirika yaliosalia, yasiokuwa ya kiserikali, ya jamii inayohudumia misaada ya kiutu Sudan yanajitahidi kuendeleza shughuli zao, kwa ushirikiano mzuri na wenye madaraka.

Mjumbe Maalumu wa Pamoja wa UM-UA kwa Darfur, Rodolphe Adada asubuhi alikutana kwenye mji wa Furawiya, Darfur ya Kaskazini kwa mazungumzo na Khalil Ibrahim, Mwenyekiti wa kundi la waasi la JEM, kwa makusudio ya kuwahimiza wafuasi wake kuyapa majadiliano ya amani umuhimu wa hali ya juu kabisa, kwa sababu, alisitiza, matatizo yaliolikabili taifa la Sudan hayana suluhu ya kijeshi katu.