Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Baraza la Usalama Ijumatatu limepitisha azimio la kuongeza muda wa operesheni za MONUC, yaani lile Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK, kwa mwaka mmoja zaidi.Vile vile Baraza lilipiga kura ya kuendeleza vikwazo dhidi ya JKK mpaka mwisho wa Novemba 2009.~

Kufuatia hapo Baraza la Usalama lilipitisha kura ya kupendekeza shughuli za Ofisi ya UM kwa Burundi ziendelea kwa mwaka mmoja zaidi. Kadhalika Baraza lilipitisha Taarifa ya Raisi, kuhusu Eneo la Maziwa Makuu na waasi wa LRA, iliounga mkono Mapatano ya Mwisho ya Amani baina ya Serikali ya Uganda na Kundi la LRA. Taarifa ilieleza kwamba inawafiki mapemdekezo ya Mjumbe Maalumu wa KM juu ya suala hilo, Joaquim Chissano, ya kutositisha zile juhudi za upatanishi baina ya makundi yanayohasimiana. Wakati huo huo Baraza limemshtumu vikali kiongozi wa LRA, Joseph Kony, kwa kushindwa, mara chungu nzima, kuhudhuria utiaji sahihi wa Mapatano ya kusitisha mapigano na amani, na pia Baraza limelaani mashambulio ya karibuni, ya waasi wa LRA, katika JKK na Sudan Kusini.

Alasiri Baraza la Usalama limepitisha azimio la kuongeza, kwa mwaka mmoja, shughuli za ule utaratibu wa kuweka fedha za mapato ya kuuza mafuta na gesi ya taifa, kwenye Mfuko wa UM juu ya Maendeleo kwa Iraq. Kuanzia Ijumanne Baraza la Usalama limemaliza mijadala yake kwa 2008.

Mjumbe maalumu wa KM kwa Eneo la Maziwa Makuu, Olusegun Obasanjo ametumia Mjumbe Maalumu wa KM kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Alan Doss taarifa iliobainisha kwamba duru ya mazungumzo ya karibuni ya upatanishi, kati ya Serikali ya JKK na kundi la waasi la CNDP, yalikuwa “magumu lakini yana matumaini.”

Ndege iliochukua misaada na vifaa vya kuhudumia afya, iliofadhiliwa na Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), imewasili Harare, Zimbabwe kwa madhumuni ya kuhudumia matibabu raia walioathirika na maradhi ya kipindupindu, yaliofumka nchini mwao katika miezi ya karibuni. UNICEF sasa hivi inahudumia asilimia 70 ya madawa muhimu katika Zimbabwe.

Mnamo mwisho wa wiki iliopita Shirika Mseto la Amani kwa Darfur la UM/UA (UNAMID) limepokea jumla ya wanajeshi 85 kutoka Pakistan, wanaojumlisha Kampuni ya Wanajeshi Wahandisi. Wenziwao wengine 176 wanatazamiwa pia kuwasili wiki hii katika Darfur. Wanajeshi hawa wahandisi watashiriki kwenye ujenzi wa “kambi kuu” ya vikosi vya kimataifa katika El Geneina, Darfur Magharibi, hudyuma itakayosaidia kupanua miundombinu inayohitajika kuimarisha operesheni za vikosi mseto vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kwa Darfur (UNAMID).