Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM na Mwendesha Mashitaka wa ICTY waipongeza Serbia kwa kumshika R. Karadzic

KM na Mwendesha Mashitaka wa ICTY waipongeza Serbia kwa kumshika R. Karadzic

KM wa UM Ban Ki-moon, kwenye taarifa iliotolewa kupitia msemaji wake, alinakiliwa akisema kushikwa kwa Radovan Karadzic kilikuwa ni kitendo cha "kihistoria, hasa kwa waathiriwa" wa jinai ya vita aliyotuhumiwa kuiongoza manjo huyo alipokuwa mkuu wa Waserb katika Bosnia-Herzegovina.

Serge Brammertz, Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya ICTY alisema yeye kwa upande wake anaamini siku aliyotiwa mbaroni Karadzic ilikuwa ni siku itakayohishimiwa sana na waathiriwa wa mateso ya vita katika Bosnia-Herzegovina, umma ambao umeisubiri siku hii kwa hamu na ghamu kwa zaidi ya miaka kumi. Alisema siku hiyo pia ni siku muhimu kwenye sheria ya kimataifa kwa kuthibitisha kihakika kwamba "hakuna mtu atakayenusurika ulimwenguni na adhabu za sheria baada ya kutuhumiwa na mahakama za kimataifa, maana watoro wa haki, mwishowe, ni lazima watakabili haki."