Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO imelaani mauaji ya mwandishi habari Usomali

UNESCO imelaani mauaji ya mwandishi habari Usomali

Koichiro Matsuura, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ameshtumu vikali mauaji yaliotukia wiki iliopita nchini Usomali ya Bashir Nor Gedi, mwandishi habari na mkurugenzi wa steshini maarufu ya redio Shabelle iliopo kwenye mji wa Mogadishu. Marehemu Gedi alipigwa risasi mbele ya nyumba yake mnamo tarehe 19 Oktoba na mhalifu asiyejulikana. Matsuura alionya kwamba wauaji wahalifu wanaonuia kufunga midomo ya wanahabari na vyombo vya habari humalizikia kudhoofisha na kutengua haki isiofutika ya umma kuwa na mawazo huru, kufikiri na kuamua wanachotaka bila ya vitisho.

Bashir Nor Gedi alikuwa mwanahabri wa nane kuuliwa Usomali katika mwaka huu, kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na Jumuiya ya Kimataifa ya Kubadilishana Maoni Huru, taasisi ambayo pia imeripoti kwamba baadhi ya waandishi habari wa vyeo vya juu wa steshini ya redio Shabelle wamelazimika kuhama Mogadishu baada ya kutukia mashambulio ya karibuni dhidi ya wafanyakazi wenziwao.