Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO: Kiswahili kitumike katika udhibiti wa mifumo ya kidijitali

Siku ya lugha ya Kiswahili duniani
UN News
Siku ya lugha ya Kiswahili duniani

UNESCO: Kiswahili kitumike katika udhibiti wa mifumo ya kidijitali

Masuala ya UM

Heri ya siku ya lugha ya Kiswahili msomaji wetu mpendwa.

Katika siku hii adhimu kwa wazungumzaji na wadau wa Kiswahili tunashuhudia wadau mbalimbali wakikusanyika na kusherehekea siku hii kwa namna mbalimbali ikiwemo makongamano ambako wanajadili namna bora ya kusongesha lugha hii kimataifa na pia kujadili fursa ziletwazo na lugha hii baada ya kutambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa.

Nikukumbushe tu Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 01 Julai 2024 lilipitisha azimio la kuitambua rasmi tarehe 7 Julai kuwa siku ya lugha ya Kiswahili duniani. Unaweza kusoma taarifa hiyo kwa kubofya hapa. Hapo awali siku hii ilikuwa ikitambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimus Sayansi na Utamaduni UNESCO pekee.

Katika salamu zake za mwaka huu za siku hii Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amezungumza mengi juu ya siku hii ikiwemo kuzungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 duniani kote pamoja na kuwa lugha rasmi ya Muungano wa Afrika- AU na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC. Pia ameeleza namna lugha hii inavyojumisha maneno kutoka katika lugha nyingine hasa kiarabu. Pia ameeleza Kiswahili kimavyotumika kimataifa akitolea mfano neno ‘Safari” ambalo linatumika hata kwa kiingereza.

“Kiswahili hakisimulii tu hadithi ya mazungumzo kati ya lugha, bali pia mazungumzo kati ya watu na nchi. Kwa hakika, kwa sababu Kiswahili kina maneno na dhana na lugha nyingine zinazo shabihiana za Kiafrika, kina nguvu ya kuvutia ya kuunganisha.” Amesema Bi. Azoulay na hii ndio sababu kubwa Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika zote zimechagua Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha zao rasmi. “Kwa njia hii, Kiswahili kina jukumu katika kuhakikisha bara la Afrika linafikia uwezo wake kamili - lengo ambalo UNESCO pia inashughulikia kama kipaumbele chake kwa Afrika.” Aliongeza Mkuu huyo wa UNESCO.

Mbali na kuwa lugha ya biashara, diplomasia na umoja, Kiswahili pia ni chanzo kikubwa cha kujieleza kitamaduni. Kwa maana inajumuisha dhana kama vile "amani". "Amani" haieleweki tu kama kutokuwepo kwa migogoro, lakini pia kama hali ya utulivu na hili ni jambo la kuendelea kufanyia kazi - maono ambayo yanashambihiana na dhana ya UNESCO ya amani kama njia bora ya kishi vyema.

“Nguvu hii ya kukuza mawasiliano na amani lazima ihifadhiwe - hasa katika kukabiliana na mapinduzi ya kidijitali. Ndiyo maana UNESCO imejitolea kuhakikisha kwamba uwezo wa Kiswahili pia unatimizwa mtandaoni. Kwa nini, katika jitihada zetu za kubuni miongozo ya udhibiti wa mifumo ya kidijitali, tunaangazia umuhimu wa anuwai ya lugha katika kusahihisha maudhui, ili kukabiliana vyema na matamshi ya chuki na habari potofu, huku zikikuza uhuru wa kujieleza na haki za binadamu.” Amesema Bi.Azoulay

Mkuu huyo wa UNESCO amehitimisha ujumbe wake wa siku hii la lugha ya Kiswahili duniani kwa kusema “tusherehekee urithi wa lugha na lugha za utajiri wa kitamaduni zinazowasilisha. Wacha tujitolee kulinda anuwai ya lugha ili kuelezea maadili na maono yetu ya ulimwengu kwa kiwango cha kibinafsi, na kukuza amani na kuwezesha ushirikiano katika kiwango cha kijamii.”

Siku njema ya kimataifa ya lugha ya Kiswahili!