Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tushikamane sasa tusongeshe kiswahili kwani kinatambulika kimataifa

Profesa Ida Hadjivayanis, Mmoja wa wanajopo akizungumza wakati wa maadhimisho ya tatu ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa.
Umoja wa Mataifa
Profesa Ida Hadjivayanis, Mmoja wa wanajopo akizungumza wakati wa maadhimisho ya tatu ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Tushikamane sasa tusongeshe kiswahili kwani kinatambulika kimataifa

Utamaduni na Elimu

Ukumbi wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa leo lilisheheni shamrashamra za maadhimisho ya tatu ya lugha ya Kiswahili duniani huku watoto wakitumbuiza kwa lugha ya Kiswahili na wageni waalikwa wakisikia kutoka kwa wabobezi wa kusongesha lugha ya Kiswahili duniani kupitia sanaa na tasnia nyinginezo.

Washiriki pia walipata ujumbe kutoka kwa viongozi wa nchi akiwemo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye kupitia ujumbe wake kwa njia ya video na katika lugha ya Kiswahili amesema  “itakuwa sahihi nikisema kiswahili ni lugha ya ukombozi, ni lugha ya umoja, ni lugha ya amani na ni lugha ya biashara.

Hivyo ametoa rai kwa viongozi wengine duniani kukitumia Kiswahili katika kukuza mtangamano, kujenga na kulinda amani na mshikamano, kufundisha vijana na watoto elimmu na maadili mema na kukuza biashara miongoni mwa nchi zao.

“Kiswahili ni fursa ya kufanikisha malengo ya maendeleo ya nchi, bara la Afrika na dunia kwa jumla, nawatakia maadhimisho mema ya siku hii adhimu,” ametamatisha Rais Samia huku akiwashukuru waliomsikiliza.

Rais Museveni atumia mfano wa binadamu kujenga mnara wa Babeli

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni akihutubia kwa njia ya video kutoka Uganda alitoa hotuba yake akirejelea maandiko ya kidini pale binadamu walipokuwa wakizungumza lugha moja wakataka kujenga mnara wa Babeli ili kufikia mbinguni.

“Hadithi ya binadamu huko Babeli haidhihirishi upumbavu wa binadamu dhidi ya Muumba, bali inadhihirisha pia nguvu ya kuzungumza lugha moja. Lugha moja ni muhimu katika kujenga mshikamano wa kiutamaduni baina ya watu wenye misingi tofauti ya kikabila na kijamii.”

Hivyo amesema kama kigiriki kilivyokuwa lugha ya himaya ya kigiriki na kiingereza lugha ya himaya ya Uingereza, “na sisi huko Afrika ya Mashariki na Afrika tuna bahati ya kuwa na lugha ambayo si lahaja ya kikabila, ni lugha ya kiswahili.”

Profesa Ida Hadjivayanis kutoka Chuo Kikuu SOAS cha London, Uingereza anaeleza namna fasihi ya Kiswahili na tafsiri zake zinavyoweza kusaidia kusambaza lugha ya Kiswahili Akieleza kwamba kuna kazi chache za fasihi ya Kiswahili ambazo zimeweza kupenya nje ya mipaka ya uswahili “na tunapaswa kufanya zaidi.”

Profesa huyo ambaye amefanya kazi kubwa ya kutafsiri baadhi ya vitabu maarufu kama anaeleza kuwa tafsiri za fasihi katika kipindi chan yumba katika jamii za Kiswahili zilizoka katika vitabu vya kiingereza kwenda katika Kiswahili lakini kwa hakika kuna kazi nyingi za waandishi wa Kiswahili ambazo hazijasomwa na hadhira ya mataifa mengine.

“Fasihi ya Kiswahili haina nafasi kubwa kimataifa na hii haitokani na ukosefu wa maandishi katika lugha hiyo. Tunayo maandishi kutoka katika karne ya 17 kwa mfano utenzi wa Hamziya.”

Profesa Ida pamoja na mambo mengine anatoa ushauri kwamba:

Mosi, lugha ya Kiswahili ipewe kipaumbele katika masomo ya elimu kote duniani.

Pili, kuhusisha lugha ya Kiswahili na utaalamu wa kisanii katika ulimwengu wa taaluma, “kwani itashadadia kutahaminiwa kwa lugha ya Kiswahili katika sanaa za tofauti.”