Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yataka mabaharia walindwe na kutotekwa

Nayomi Amarasinghe alikuwa mwanamke wa kwanza baharia wa Sri Lanka, baada ya kushiriki katika mafunzo yanayoungwa mkono na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
© ILO
Nayomi Amarasinghe alikuwa mwanamke wa kwanza baharia wa Sri Lanka, baada ya kushiriki katika mafunzo yanayoungwa mkono na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

UN yataka mabaharia walindwe na kutotekwa

Ukuaji wa Kiuchumi

Leo ni siku ya mabaharia duniani ambayo mwaka huu unapigia chepuo usalama wao mahala pa kazi.

Katika Ujumbe wake kwa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni muda wa kusherehekea na kutambua watu milioni mbili duniani ambao wanafanya kazi katika meli ambao hubeba zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa za biashara dunia.

Mabaharia wanajukumu muhimu katika kuhakikisha mtiririko mzuri wa bidhaa muhimu ambazo hatimaye zitaenda masokononi, majumbani na mezani na bila wao, ulimwengu haungeweza kusafirisha idadi kubwa ya bidhaa ambazo jamii zinahitaji ili kuishi.

Pamoja na umuhimu wao huo Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kuweka maisha yao mashakani.

“Mashambulizi kwenye njia za kimataifa za usafirishaji na vitendo vya uharamia havikubaliki. Meli na mabaharia hawapaswi kutekwa nyara na wala meli zao kutekwa. Mabaharia hawapaswi kuwa waathirika wa migogoro mikubwa ya kijiografia na kisiasa.” Amesema Guterres.

Mabaharia kote ulimwenguni ni chanzo cha mapato kwa familia zao wanapokuwa kwenye safari ndefu baharini hivyo kwa pamoja jamii inapaswa kuwapa shukran kwa kazi yao muhimu na kuunga mkono usalama wao.

Kampuni za usafirishaji zinafanya kazi kuelekea usafiri endelevu wa baharini kama sehemu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu.
© MSC shipping
Kampuni za usafirishaji zinafanya kazi kuelekea usafiri endelevu wa baharini kama sehemu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Mkuu wa IMO awashukuru kwa kazi nzuri

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya bahari, IMO Arsenio Dominguez anawatakia kila la heri wanabaharia wote akiwaalika katika meza ya kubonga bongo kuhusu masuala ya usalama wa baharini.

"Tunajua kuwa bila mabaharia, hakungekuwa na usafirishaji wa baharini, hakungekuwa na ununuzi na mnyororo wa usambazaji wa bidhaa. Wasafirishaji wa baharini wamethibitisha taaluma yao siku baada ya siku kote ulimwenguni, lakini mbali na mtazamo wa umma, wakihimili changamoto za kulengwa na waasi baharini.”

Mkuu huyo wa IMO ameeleza kutambua ujasiri na kujitolea kwao na kutambua nguvukazi yao

“Nimewaona mkifanya kazi kwenye sitaha na chini, katika vyumba vya uhandisi, kwenye madaraja, kwenye usambazaji na katika mahali pa kuhifadhi mizigo, mkichangia katika njia kuu zaidi za usafiri duniani, mkihakikisha viwango vya juu zaidi vya usalama, huku mkiwa tayari kushughulikia hali zote za dharura.”

Amehitimisha ujumbe wake wa siku hii kwa kuwataka mabaharia wote duniani kushirikiana, kujadili usalama wa mazingira yao ya kazi, usalawa wa baharini, na kufahamishana jinsi wanavyoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na uvumbuzi, ili kubaki salama ndani ya baharia, na bila kusahamu kueleza jinsi wanavyokabiliana na changamoto za afya ya akili.