Mapigano na mizozo DR Congo yanyima wananchi manufaa ya utajiri wa nchi yao - Türk
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Türk ambaye yuko katika ziara rasmi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amestaajabu ni kwa vipi utajiri wa maliasili uliosheheni kwenye taifa hilo umeleta manufaa kidogo kwa wananchi wako kutokana na ghasia na mapgano. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.
Video ya Umoja wa Mataifa inaanzia Kinshasa mji mkuu wa DRC ambako Bwana Türk na aafisa mmoja wa Umoja wa Mataifa wanatazama ramani ya taifa hilo lililoko Maziwa Makuu na kisha anasema ni moja ya nchi tajiri zaidi duniani, lakini tunaona ni kwa vipi utajiri huu kwa bahati mbayá hauko kunufaisha wananchi kwa sababu ya mapigano.
Na kisha anaelezea mipango ya ziara yake ya kutathmini hali ya haki za binadamu akisema kwanza ni kukutana na watu waliofurushwa makwao kutokana na ghasia na vile vile kuonana na mamlaka husika na mashirika ya kiraia.
Baada ya hapo safari inaanza akiambatana na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Bintou Keita, mwelekeo ni Mashariki mwa nchi jimboni Ituri. Taswira ya angani kutoka ndege hii ya Umoja wa Mataifa na kisha wanawasili. Mapokezi hapa Bunia, kutoka kwa wenyeji wao.
Moja kwa moja msafara wao wa magari unafika kwenye kambi ya wakimbizi nje kidogo ya mji wa Bunia na wanaingia ndani ambako wanawake, wanaume na watoto, wazee na vijana, nyuso zao zinaonesha matuamini kwani wahenga walinena mgeni njoo mwenyeji apone.
Mkalimani akamweleza Turk kuwa wanachosema maeneo yao yametawaliwa na waasi na hawawezi kurejea makwao.
Na ndipo Kamishna huyu Mkuu wa Haki za Binadamu baada ya kuwasikiliza wakimbizi na kuzungumza nao akatoka nje na kusema, “Nimekutana na kundi la watu ambao wamefurushwa makwao kutokana na mauaji ya kikatili na ya kutisha yaliyotekelezwa kwenye makazi yao. Na wamekuweko hapa kwa miaka minne sasa. Tamanio lao kubwa kabisa ni kuweza kurejea makwao.”
Kwa sasa kuna takribani watu milioni 1.8 waliofurushwa makwao jimboni Ituri kati ya wakimbizi wote wa ndani milioni 7.2 nchini kote DRC.
Kesho Bwana Turk atakuwa na mazungumzo na Rais President Félix Tshisekedi na maafisa wengine wa serikali, Umoja wa Mataifa, wanadiplomasia na vyama vya siasa pamoja na watetezi wa haki za binadamu na kisha atazungumza na waandishi wa habari.