Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za mashirika zafanikisha kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5

Juhudi za mashirika zafanikisha kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5

Pakua

Idadi ya vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 duniani kote imepungua na kufikia kiwango cha chini zaidi kuwahi kufikiwa katika historia, ambapo takwimu mpya zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa mwaka 2022 idadi ya vifo ilikuwa chini ya milioni 4.9, sawa na pungufu kwa asilimia 51 tangu mwaka 2000. 

Ama hakika ni mafanikio makubwa kwani video iliyoambatana na habari hizi njema inaonesha madaktari, wakunga, wahudumu wa afya wakiwemo wale wa kijamii huko, Afrika, wakijituma kwa dhati kutoa huduma kuanzia kwa wajawazito, huduma za mama na mtoto hadi chanjo.

Mathalani Sierra Leone anaonekana mhudumu wa afya akifika moja ya kaya kutoa huduma ya chanjo dhidi  ya Numonia au vichomi.

Cambodia, Malawi, Mongolia na Rwanda zimetajwa kuwa ni nchi ambamo idadi ya vifo vya watoto hao imepungua kwa zaidi ya asilimia 75 kati ya 2000 na 2022.

Ripoti imetolewa na kundi la mashirika na taasisi ya Umoja wa Mataifa, IGME, linaloongozwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ambalo Mkurugenzi Mtendaji wake Catherine Russell amepongeza juhudi za mtu mmoja mmoja, serikali, wakunga, wahudumu wa afya wakiwemo wale wa kijamii.

Amesema kujituma kwao katika kuhakikisha watoto wanafikishiwa huduma bora na fanisi za afya tena kwa gharama nafuu, kumethibitisha kuwa dunia ina ufahamu na mbinu za kuokoa maisha.

Licha ya mafanikio hayo, ripoti inaonya kuwa bado safari ni ndefu kufikia lengo la kutokomeza vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika, kwa kuwa mamilioni wanaendelea kufariki dunia kutokana na magonjwa yanayotibika, changamoto za ujautizo, vichomi au numonia, kuhara na malaria.

Idadi kubwa ya vifo hivyo ni katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara na kusini mwa Asia, hali inayodhihirisha tofauti za kikanda katika upatikanaji wa huduma bora za afya.

Ripoti imetambua pia ukosefu wa utulivu kiuchumi, mizozo, mabadiliko ya tabianchi na changamoto zilizoachwa kutokana na janga la coronavirus">COVID-19, ikisema mambo hayo yanazidi kuchochea tofauti za usawa kwenye utoaji wa huduma za afya.

Kundi hilo linaitwa IGME na linajumuisha mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuhudumia watoto, UNICEF, la afya, WHO, Benki ya Dunia na kitengo cha Idadi ya Watu cha Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii, DESA.

IGME ilianzishwa mwaka 2004 kuwezesha wasihrika kubadilishana takwimu na kuboresha mbinu kwa ajili ya takwimu za vifo vya watoto na kufuatilia maendeleo kuelekea kufikia malengo kuhusu uhai wa mtoto.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Sauti
2'8"
Photo Credit
© UNICEF/Mulugeta Ayene