Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bintou Keita: Nina wasiwasi mkubwa na ukikukwaji wa haki za binadamu katika maeneo yanayokaliwa na M23

Bintou Keita: Nina wasiwasi mkubwa na ukikukwaji wa haki za binadamu katika maeneo yanayokaliwa na M23

Pakua

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Bintou Keita, ameliambia Baraza la Usalama kwamba ana wasiwasi mkubwa kutokana na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa unaofanywa katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa M23, ambapo vuguvugu hilo linalenga watendaji wa mashirika ya kiraia, hasa watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari. 

Akihutubia Baraza la Usalama lililokaa jana kuanzia saa tisa alasiri saa za New York Marekani ili kuijadili hali ya DRC, kwa njia ya video akiwa nchini DRC, Bintou Keita ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, ameeleza kinagaubaga hali ya usalama inavyozidi kudorora mashariki mwa nchi hiyo ya pili kwa ukubwa wa eneo barani Afrika.

“Idadi ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na M23 inaendelea kuongezeka, huku takriban raia 150 wakiuawa tangu kuanza tena kwa mapigano Novemba 2023, wakiwemo watu 77 Januari 2024.”

Aidha Bi. Keita akasisitiza kuhusu changamoto wanazokutana nazo MONUSCO kutokana na kuendelea kukabiliwa na wimbi la taarifa potofu na za uongo kuhusu uhusika wa MONUSCO kwenye mapigano yanayoendelea hivi sasa. 

“Kampeni za mtandaoni zinazoilenga MONUSCO zimekuwa zikifanywa na vyanzo ambavyo hasa viko nje ya DRC. Hii imesababisha vitendo vya uhasama dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa na vikwazo vya kutembea vinavyowekwa na makundi yenye silaha na askari wa serikali.”

Kwa mujibu wa Mwakilishi huyo maalumu wa Katibu Mkuu nchini, zaidi ya watu 400,000 waliokimbia makazi yao karibu na mji wa Goma sasa wametafuta hifadhi katika mji huo, wakiwemo watu 65,000 katika wiki mbili zilizopita, na hivyo kusababisha ongezeko kubwa la wagonjwa wa kipindupindu kutokana na ukosefu wa maji safi ya kunywa na usafi wa jumla wa mazingira.

Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
2'10"
Photo Credit
© UNHCR/Blaise Sanyila