Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

25 JANUARI 2024

25 JANUARI 2024

Pakua

Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina ambayo inamulika hali ya kibinadamu na ya kiafya katika ukanda wa Gaza. Pia tunakuletea habari kwa ufupi tukisalia huko huko Gaza, machafuko nchini Sudan na ya siku ya kimataifa ya wanawake katika ushirikiano wa kimataifa. Katika kujifunza lugha ya Kiswahili tunakuletea ufafanuzi wa neno “KUWEKUA”.

  1. Mashambulizi makubwa dhidi ya majengo Gaza ambayo raia wenye hofu wanakimbilia kupata hifadhi ni "ya kuchukiza na lazima yakome mara moja", amesisitiza Thomas White naibu mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika eneo hilo linalokaliwa la Gaza baada ya leo, kombora kuanguka katika kituo cha mafunzo cha Umoja wa Mataifa.. 
  2. Sudan inakaribia kuwa moja ya janga baya zaidi la elimu duniani ameonya mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini humo Mandeep O’Brien. Katika mahojiano maalum na UN News kwa njia ya mtandao Bi. O’Brien amesema Sudan inakabiliwa na janga la kibinadamu lisiloelezeka na ni jinamizi kwa watoto kwani  watoto "Milioni 14 wanahitaji haraka msaada wa kuokoa maisha wa afya, lishe, elimu, maji na ulinzi. Pili, tunapozungumza, tunajua kwamba zaidi ya watoto milioni 3.5 wamelazimika kukimbia makazi yao tangu vita hii ianze na hii inaifanya Sudan kuwa taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watoto waliokimbia makazi yao duniani”. Sudan ina watoto milioni 19 wenye umri wa kwenda shule ambao sasa hawasomi.
  3. Na leo ni siku ya kimataifa ya wanawake katika ushirikiano wa kimataifa. Mwaka huu 2024 inaadhimishwa chini ya kaulimbiu “Usawa wa kijinsia katika kutatua dharura ya mabadiliko ya tabianchi.” Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO ambalo linasimamia siku hii, limesema lengo lake ni kutambua wanawake viongozi katika mfumo wa kushirikiano wa kimataifa ili kuchagiza mazungumzo kuhusu suluhu za kimataifa dhidi ya ubaguzi wa kijinsia ambao unakwamisha hatua dhidi ya dharura ya mabadiliko ya tabianchi. 
  4. Katika kujifunza lugha ya Kiswahili  leo ukumbi ni wake mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa  nchini Tanzania, BAKITA anafafanua maana ya neno “KUWEKUA”.      

Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
13'10"