Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufugaji nyuki ‘waua’ ndege zaidi ya mmoja, yasema FAO - Zimbabwe

Ufugaji nyuki ‘waua’ ndege zaidi ya mmoja, yasema FAO - Zimbabwe

Pakua

Nchini Zimbabwe, mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, wa kusongesha ajira rafiki kwa mazingira umeanzisha mashamba darasa ya ufugaji wa nyuki na hivyo kuandaa vijana kuwa wakulima wajasiriamali vijijini. Mradi huo unatekelezwa kwa ubia na shirika la Korea Kusini la Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa, KOICA. 

Pasi shaka Assumpta, naanza na Angelina Manhanzva, kijana wa kike akiwa shambani akihudumia mzinga wa nyuki anatanabaisha kuwa…(Nats) fursa inapokufikia usiipuuze kwani inaweza kubadili maisha yako katika fumba na kufumbua.  

Mjasiriamali kijana huyu kutoka wilaya ya Chegutu jimboni Mashonaland kaskazini-kati mwa Zimbabwe anakiri kuwa baada ya kushiriki kwenye ufugaji wa nyuki kwa miezi kadha wameshuhudia maisha yao  yakibadilika.  

Barnabas Mawire, mtaalamu wa maliasili wa FAO nchini Zimbabwe anasema, “Wazo ni kwamba, eneo moja lenye mizinga ya nyuki linaweza kugeuzwa kuwa shamba darasa  ambako vijana kutoka wilaya au kata tofauti wanaweza kuja kujifunza kama waendavvyo shuleni .”  

FAO inasema kuwa kupatia vijana wa vijijini ajira zisizoharibu au kuchafua mazingira kunaweza kukabili madhara ya mabadiliko ya tabianchi, kuondoa umaskini na kutokomeza umaskini wa vijijini. Mkulima mjasiriamali kijana Evelyne Mutuda naye anakiri faida inapatikana na kwamba, "Tunatarajia kuongeza mizinga mingine ya nyuki kwa kutumia faida  ya fedha tuliyopata baada ya kuuza asali.  Na pia tutapanda mijakaranda .”   

Akitamatisha afisa wa FAO, Bwana Mawire anadhihirisha uhusiano wa ufugaji nyuki na ulinzi wa bayonuai.  

“Nyuki wanafaa sana kwa ajira zisizoharibu mazingira kwa mantiki kwamba wanahitaji aina mbali mbali za mimea . Kwa hiyo nyuki wanasongesha uhifadhi wa bayonuai. Unapotunza miti, unatunza tabianchi yetu,  chakula chetu na uhai wetu.  Hivyo ufugaji nyuki unanufaisha kwa juhudi kidogo.”  

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
2'12"
Photo Credit
© FAO/Zinyange Auntony