Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwasilishaji misaada kaskazini mwa Gaza umezuiliwa na vizingiti vya kufikisha misaada ya kibinadamu

Uwasilishaji misaada kaskazini mwa Gaza umezuiliwa na vizingiti vya kufikisha misaada ya kibinadamu

Pakua

Wasaidizi wa kibinadamu wanatoa wito wa fursa ya ufikishaji misaada kwa haraka, salama, endelevu na usiozuiliwa kaskazini mwa Gaza kwani hali ya binadamu inazidi kuwa tete. 

Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu wameshindwa kutoa msaada unaohitajika haraka wa kuokoa maisha kaskazini mwa Wadi Gaza kwa siku nne kutokana na ucheleweshaji na kukataliwa, pamoja na migogoro inayoendelea imeeleza Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura OCHA katika taarifa yake iliyokusanya takwimu za hadi jana Jan 4 na kuchapishwa leo Jan 5.  

Hii ni pamoja na dawa ambazo zingetoa msaada muhimu kwa zaidi ya watu 100,000 kwa siku 30, pamoja na lori nane za chakula kwa watu ambao kwa sasa wanakabiliwa na uhaba wa chakula unaohatarisha maisha.  

Kwa upande wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), linasema maelfu ya watoto tayari wamekufariki dunia kutokana na ukatili huo unaoendelea, huku hali ya maisha kwa watoto ikiendelea kuzorota kwa kasi. 

"Watoto huko Gaza wanakumbwa na jinamizi ambalo linazidi kuwa baya kila kukicha," anasema Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF na kuongeza kuwa, “Watoto na familia katika Ukanda wa Gaza wanaendelea kuuawa na kujeruhiwa katika mapigano, na maisha yao yanazidi kuwa hatarini kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika na ukosefu wa chakula na maji.” Anatoa wito kwamba watoto na raia wote lazima walindwe dhidi ya unyanyasaji na kupata huduma za kimsingi. 

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO) linaeleza kamba tangu tarehe 24 Desemba 2023, limethibitisha mashambulizi manane kwenye hospitali ya Al-Amal, mashambulizi yaliyoua watu 7 na kujeruhi 11. Mashambulizi ya karibu zaidi ni ya jana Januari 4. Tangu Oktoba 7 mwaka jana, WHO imethibitisha mashambulio 590 dhidi ya huduma za afya katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.  

Pamoja na hali hii ngumu, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kusaidia watu katika kila hali inavyowezekana ijapokuwa ni katika hali hatarishi. Kufikia juzi tarehe 3 Januari, jumla ya wafanyakazi 142 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina (UNRWA) wameuawa tangu kuanza kwa mapigano hapo Oktoba 7.  

Audio Credit
Anold Kayanda
Sauti
1'50"
Photo Credit
© UNICEF/Abed Zagout