Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunaadhimisha siku hii nyakati za kiza kwa watu wa Palestina - Guterres

Tunaadhimisha siku hii nyakati za kiza kwa watu wa Palestina - Guterres

Pakua

Umoja wa Mataifa leo umeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina, katika nyakati ambazo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameziita mojawapo ya nyakati za kiza katika historia ya watu wa Palestina na hivyo akasisitiza mshikamano zaidi na kutafuta suluhu ya kudumu. 

Bwana Antonio Guterres kupitia ujumbe wake mahususi kwa ajili ya siku hii ya kimataifa ya mshikamano na watu wa Palestina, kwa njia ya maandishi amesema zaidi ya yote yanayoendelea, hii ni siku ya kuthibitisha mshikamano wa kimataifa na watu wa Palestina na haki yao ya kuishi kwa amani na utu. 

Guterres ameendelea kusisitiza suluhisho la Serikali mbili, kwa msingi wa maazimio ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, ili Israeli na Palestina ziishi kwa pamoja kwa amani na usalama na mji wa Jerusalem uwe mji mkuu wa Mataifa yote mawili. 

“Umoja wa Mataifa hautayumba katika kujitolea kwake kwa watu wa Palestina,” anahitimisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihimiza kuwa leo na kila siku, ulimwengu usimame katika mshikamano na matarajio ya wananchi wa Palestina kufikia haki zao zisizoweza kupokonywa na kujenga mustakbali wa amani, haki, usalama na utu kwa wote. 

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA, amesema, "Mshikamano wa kimataifa tunaoueleza leo unathibitisha kwamba hitaji la haki za Wakimbizi wa Kipalestina kama ilivyoainishwa katika maazimio ya Umoja wa Mataifa, ni muhimu zaidi sasa kuliko hapo awali." Kwa hiyo anatoa wito kwa ulimwengu kushirikiana kuelekea, “haki na amani kwa Wakimbizi wa Kipalestina, ambao hawahitaji msaada tu, bali suluhisho la haki na la kudumu." 

Maadhimisho ya mwaka huu ya Siku hii ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina, kwa Umoja wa Mataifa yamefanyika katika makao makuu jijini New York, Marekani, Geneva Uswisi, Vienna Austria na Nairobi Kenya. 

Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina huadhimishwa na Umoja wa Mataifa kila tarehe 29 Novemba kila mwaka, kwa mujibu wa mamlaka za Baraza Kuu katika maazimio 32/40 B ya 2 Desemba 1977, na 34/65 D ya 12 Desemba 1979 na maazimio yaliyofuata yaliyopitishwa chini ya kipengele cha ajenda "Suala la Palestina." 

Tarehe 29 Novemba ilichaguliwa kwa sababu ya maana na umuhimu wake kwa watu wa Palestina. Siku hiyo ya 1947, Baraza Kuu lilipitisha azimio namba 181 (II), ambalo lilikuja kuitwa Azimio la Kugawanyika. Azimio hilo lilitoa fursa ya kuanzishwa huko Palestina "Nchi ya Kiyahudi" na "Nchi ya Kiarabu", na Jerusalem kama mji mkuu wa pamoja chini ya utawala maalum wa kimataifa. Kati ya Mataifa mawili yaliyopitishwa kuundwa chini ya azimio hili, ni moja tu, Israeli, ambalo limeundwa hadi sasa. 

Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
1'47"
Photo Credit
UN News/Ziad Taleb