Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake na wasichana wajawazito walioko Gaza wasimulia kinachowakumba

Wanawake na wasichana wajawazito walioko Gaza wasimulia kinachowakumba

Pakua

Wakati mzozo katika Ukanda wa Gaza ukizidi kuongezeka huku wananchi wakikabiliwa na changamoto nyingine lukuki ikiwemo uhaba wa chakula, maji, mafuta na vifaa vya matibabu vya kuokoa maisha, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu na Afya ya Uzazi UNFPA limesema mfumo wa afya nao uko ukingoni kuanguka. Shirika hilo limezungumza na wanawake wajawazito walioko Gaza kuhusu hali mbaya wanayokabiliana nayo. Thelma mwadzaya anatujuza walichosema wanawake hao. 

Ukanda wa Gaza makazi ya watu milioni 2.2, wanawake 50,000 ni wajawazito hivi sasa katika eneo ambalo vita inaendelea. UNFPA imesema takriban wanawake 5,500 wanatakiwa kujifungua ndani ya siku 30 zijazo na takwimu za sasa idadi ya wanawake wanaojifungua kila siku ni 160. 

Wakati wanawake 840 wanaweza kuwa na changamoto wakati wa kujifungua, wengi wa wanawake walioko Gaza wamekatishwa huduma za uzazi salama, kwani hospitali, ambazo zimeelemewa na majeruhi, zinakosa mafuta ya jenereta, dawa na vifaa muhimu ikiwa ni pamoja na usimamizi wa dharura za uzazi.

Hizi ndio simulizi za madhila wanayokutana nao wanawake hawa ambao hatutataja majina yao. 

Wakwanza anatueleza hali ilivyo “Kila mara kuna bomu, naogopa, miguu yangu inapooza, siwezi kutembea, siwezi kusogea, hasa ukizingatia nina watoto na nahitajika kukimbia kwenda kuwafuata, haya ni mateso zaidi ya changamoto zinazo tukabili kwasababu ya ardhi yetu kutwaliwa. Ninaogopa, sababu ya watoto wangu na mtoto wangu aliye tumboni ambaye hajazaliwa.”

Huyu wa pili, nyumba yao ililipuliwa na mabomu yanayorushwa na Israel, anasema “Natarajia kujifungua mwezi huu, ninalala mitaani kama ulivyonikuta, hali haivumiliki hapa” 

Na watatu, naye amepata hifadhi katika shule zinazo endeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina UNRWA.

“Hii ndio sehemu pekee ambayo tumeambiwa ina usalama, niña ujauzito wa miezi saba. Hali hapa inasikitisha, unaweza kuisikia hata kwenye sauti yangu. Kifua kinaniuma, niña mafua makali na niña kohoa na hakuna maji kabisa, tunajaribu kuosha vyakula lakini maji si masafi, hata maji kitone tunayofanikiwa kuyapata si masafi. Ninachotaka ni usalama, mazingira salama ya afya, suala kubwa zaidi sasa ni kusafisha vyoo na kupata vifaa vya usafi, maji ni muhimu kwetu hali ni mbaya sana kwetu.”

Tayari UNFPA imetuma dawa na vifaa vya afya ya uzazi vya kuokoa maisha nchini Misri kwa ajili ya kuhifadhi na kusafirishwa kuvuka mpaka hadi Gaza. Hadi kufikia tarehe 26 Oktoba, UNFPA ilifikisha nchini Misri vifaa 3,000 vya usafi na kujihifadhi kwa ajili ya wanawake pamoja na wajawazito. 

Audio Credit
Thelma Mwadzaya
Sauti
3'9"
Photo Credit
© Ziad Taleb