Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fahamu nini kinaweza kufuatia pindi maazimio yanagonga mwamba Baraza la Usalama la UN

Fahamu nini kinaweza kufuatia pindi maazimio yanagonga mwamba Baraza la Usalama la UN

Pakua

Mzozo wa Mashariki ya Kati ukiendelea kati ya Israeli na kundi la wanamgambo wa kipalestina, Hamas, hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye jukumu la kusimamia amani na usalama liko njiapanda baada ya rasimu mbili za maazimio kwa ajili ya kuchukua hatua kwenye mzozo huo kugonga mwamba! Marekani ikitumia kura turufu. Sasa nini kinafuatia? Rasimu mpya au kikao cha dharura cha Baraza Kuu? 

Bila shaka Assumpta! Ikumbukwe kuwa mzozo wa sasa huko Mashariki ya Kati alianza tarehe 7 mwezi huu wa Oktoba kwa Hamas kurusha makombora Israel.

Hali hiyo ikatinga kwenye rada za Baraza la Usalama lenye wanachama 15, watano wakiwa wa kudumu, Baraza lenye wajibu wa kusimamia amani na usalama duniani. 

Rasimu mbili ziliandaliwa zote zikiwa na lengo la pamoja na mambo mengine sitisho la mapitano na kupatikana kwa njia ya kupitisha misaada ya kibinadamu. Ya kwanza ikiwasilishwa na Urusi haikupata kura za kutosha kuweza kupitishwa, ya pili iliyowasilishwa na Brazili, ilipigiwa kura turufu na Marekani

Marekani, China, Urusi, Ufaransa na Uingereza zina ujumbe wa kudumu Barazani hivyo zina kura turufu au veto ambayo ikitumika rasimu haipiti hata ikipata kura tisa ambazo zinahitajika azimio kupita. 

Kura turufu ilipatiwa wajumbe hao wa kudumu punde tu baada ya Baraza kuanzishwa mwishoni mwa vita kuu ya pili ya dunia. Hadi sasa harakati za kupanua wigo wa umiliki wa kura hiyo zimegonga mwamba. 

Lakini wajumbe wa Baraza wanaweza pia kumaliza tofauti zao kwenye lugha ya rasimu na kisha kuwasilisha rasimu nyingine Barazani ili ipigiwe kura. Hiyo itakuwa heri!! 

Nafasi ya Baraza Kuu 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa nalo lina nafasi yake ambapo kwa ombi la nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Baraza hilo Kuu anaweza kuitisha kikao rasmi ndani ya siku 10 tangu mjumbe mmoja au zaidi atumie kura tufuru kuzuia azimio.  

Na kumbuka Marekani ilitumia turufu yake kuzuia rasimu ya azimio juu ya mzozo wa Israel na Palestina, hivyo Baraza lina hadi tarehe Mosi mwezi ujao wa Novemba kuitisha kikao hicho. 

Hatua nyingine pia inayoweza kufuatia ni kwa nchi wanachama kumuomba Rais wa Baraza Kuu kuitisha mjadala kuhusu mazingira ambamo kwayo kura hiyo turufu ilitumika. Lakini ni vema kutambua kuwa Baraza hilo halikutani kwa kile ambacho aghalabu huitwa kikao maalum cha dharura juu ya suala moja. 

Lengo ni kutoa mapendekezo ikiwemo uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi, kuendeleza au kurejesha amani na usalama kwenye eneo husika. Halikadhalika kusitisha mapigano na mahitaji yafikie walio kwenye shida. 

Na ukiangalia ongezeko la idadi ya vifo huko Mashariki ya Kati, iwapo Rais wa Baraza ataombwa kuitisha kikao kutokana na kura ya wajumbe wowote 7 au zaidi wa Baraza la Usalama au kwa idadi kubwa ya nchi 193 wanachama wa UN, basi Rais huyo lazima aitishe kikao maalum cha dharura ndani ya saa 24. 

Tangu Umoja wa Mataifa uanzishwe mwaka 195 kumekuweko na vikao vya aina hiyo 11 pekee, na kati ya hivyo, vitano (5) vilihusu Mashariki ya Kati.  

Kikao cha mwisho kilikuwa Februari mwaka 2022, siku 6 baada ya Urusi kuvamia Ukraine. 

Lakini wengine wanauliza, mkwamo ndani ya Baraza la Usalama unamaanisha Umoja wa Mataifa umefungwa mikono hauwezi kutekeleza majukumu yake? La hasha!  

Kwa sasa harakati za kidiplomasia na kibinadamu zinaendelea tangu kulipuka kwa mzozo huo ambapo Katibu Mkuu na wasaidizi wake wako tayari Mashariki ya Kati, huku mashirika yakiendelea kuhakikisha misaada ya kiutu inafikia wahusika. 

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
3'51"
Photo Credit
© UNICEF/Eyad El Baba