Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dkt. Tedros - Tunaishi mara moja na tuna ini moja, tutokomeze Homa ya Ini

Dkt. Tedros - Tunaishi mara moja na tuna ini moja, tutokomeze Homa ya Ini

Pakua

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO) Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus kupitia ujumbe wake kwa Siku ya Kimataifa ya Homa ya Ini inayoadhimishwa kila Julai 28, amesema kwa kuwa wanadamu tunaishi mara moja na tuna ini moja, WHO imejitolea kushirikiana na nchi zote na wadau wote ili kutimiza maono ya pamoja ya kutokomeza virusi vya homa ya ini ifikapo 2030.  

“Kila mwaka, homa ya ini inayosababishwa na virusi inaua zaidi ya watu milioni moja, na zaidi ya watu milioni tatu wapya wanaambukizwa. Tunajua namba hizi ni za chini ya makadirio. Mamilioni ya watu ulimwenguni kote wana homa ya ini ambayo haijatambuliwa na ambayo haijatibiwa. Mara nyingi, ugonjwa huendelea bila kutambuliwa mpaka dalili zinakuwa mbaya.” 

Hata hivyo Dkt. Tedros anaeleza habari njema akisema, “Sasa tuna zana bora zaidi za kuzuia, kutambua na kutibu homa ya ini. Duniani kote, WHO inaunga mkono nchi kupanua matumizi ya zana hizo, ili kutokomeza homa ya ini na kuokoa maisha.” 

Anayoyasema Mkuu huyu wa WHO tayari yameanza kuzaa matunda katika baadhi ya nchi. Mathalani barani Afrika, wizara ya Afya ya Uganda, kwa msaada wa kiufundi kutoka WHO, ilibuni mkakati wa kudhibiti homa ya ini ya B, ikijumuisha uhamasishaji wa umma, upimaji na matibabu nchini kote. Hadi kufikia sasa watu milioni 4 wamefanyiwa uchunguzi wa ugonjwa huo na  zaidi ya asilimia 30 ya watu walioambukizwa homa ya ini ya B wanafahamu hali zao na wanaweza kupata huduma za matibabu ya kina, ikiwa ni pamoja na dawa za bure. 

Tags: Homa ya Ini, Virusi vya Homa ya Ini, Hepatitis, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Siku za UN 

Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
1'59"
Photo Credit
UNICEF/Ilvy Njiokiktjien