Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misaada wawasili kwa mara ya kwanza katika eneo la Donetsk Oblast Ukraine: OCHA

Misaada wawasili kwa mara ya kwanza katika eneo la Donetsk Oblast Ukraine: OCHA

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA limesema kwa mara ya kwanza misaada ya mashirika ya Umoja wa Mataifa imefanikiwa kuwasili katika eno linalodhibitiwa na serikali karibu na Soledar Mashariki mwa Donetsk Oblast nchini Ukraine.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis na OCHA msaada huo wa kibinadamu uliosheheni kwenye malori matatu ni kwa ajili ya kuwasaidia zaidi ya watu 800 ambao walisalia katika jamii zinazozunguka eneo la Soledar. 

“Msaada huo unaojumuisha chakula, maji, vifaa vya usafi na kujisafi, madawa na vifaa tiba vingine umetolewa na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la afya duniani WHO, la kuhudumia Watoto UNICEF, la uhamiaji IOM na la mpango wa chakula duniani WFP na unaratibiwa na OCHA.” 

Mashirika hayo yamesema mapigano ya hivi karibuni katika viunga vya Soledar yamesababisha uharibifu mkubwa na kuwaacha mamia ya watu kwenye eneo hilo katika hali mbaya na hivyo kutegemea msaada wa kibinadamu. 

Hii ni mara ya kwanza msafara huo wa misaada wa mashirika ya kibinadamu unawasili katika eneo hilo na OCHA inasema “ Tumeziarifu mapema pande zote katika mzozo kuhusu msafara wetu kupitia mfumo wa taarifa wa masuala ya kibinadamu.” 

Mashirika ya kibinadamu nchini Ukraine yakiratibiwa na OCHA yanajitahidi kuongeza idadi ya misafara ya misaada ya pamoja katika eneo hilo lililo mstari wa mbele wa mapambano nchini Ukraine ambako mahitaji ni makubwa.  

OCHA inasema misafara zaidi ya misaada inatarajiwa katika siku chache zijazo. 

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
1'43"
Photo Credit
Photo courtesy of Ukrainian Women’s Fund