Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani Irejee turudi makwetu: Wakimbizi wa ndani nchini Sudan

Amani Irejee turudi makwetu: Wakimbizi wa ndani nchini Sudan

Pakua

Wakati idadi ya wakimbizi wa ndani nchini Sudan ikizidi kuongezeka ambapo mpaka sasa wamefikia milioni 3.7 na kati yao 200,000 wakiwa wamerekodiwa mwaka huu pekee Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk amefunga safari mpaka nchi huko kwenda kuzungumza na wawakilishi wa wakimbizi, asasi za kiraia na serikali. 

Video ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za binadamu OHCHR inaanza kwa kuonesha taswira kutoka angani ya El Fasher mji mkuu wa Jimbo la Darfur kaskazini nchini Sudan ambapo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk anafika hapa katika ziara maalum ambayo inamkutanisha na jamii za wakimbizi wa ndani,a wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na viongozi wa serikali na wamasuala ya ulinzi.

Hii si mara yake ya kwanza kufika hapa “Miaka 11 iliyopita, nilikuwa hapa katika jengo hili hapa El Fasher Darfur, nilikuja kuendesha warsha kwa viongozi kuhusu suala la ulinzi, nikizungumzia ulinzi wa wakimbizi wa ndani na ulinzi wa raia kwa ujumla. Sasa nimerejea, kama Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu, na tunajadiliana suala lile lile kuhusu ulinzi wa raia, na uhitaji wa dharura wa kutafuta suluhu kwa wakimbizi wa ndani na kuheshimu haki za binadamu.”

Na baada ya kufanya mikutano na kusikia kutoka kwa wawakilishi wa wakimbizi wa ndani…. Na wanaharakati wa haki za binadamu….  Kamishna Turk anasema ujumbe ni mmoja tu na upo wazi kabisa, watu hawa wanataka utekelezaji wa makubaliano ya amani ya Juba, na kuhakikisha kuna amani nchini humo huku mapigano yakomeshwe na watu wawe na utashi binafsi wa kurejea makwao "Iko wazi kabisa, jamii ya wakimbizi wa ndani wenyewe wanaona. Hawa ni wakulima, ni watu wanaofanya kazi kwenye ardhi yao na wanataka kurejea kufanya hivyo kule walikokukimbia, na baada ya miaka kadhaa ya kuishi ukimbizini hilo ndilo wanalotamani, kurudi makwao.”

Na alipokutanaa na viongozi wa serikali na wale wa ulinzi ujumbe wake ni “Ni wazi kwamba njia ya kuwezesha kusonga mbele tunahitaji ulinzi na kuhamasisha utekelezaji wa haki za binadamu kwa kila mtu katika eneo hili iwe ndio kipaumbele cha juu kabisa.”

Kamishna huyo pia alipata fursa ya kuzungumza na vyombo vya Habari vya nchini humo na kusisitiza ujumbe wake wa amani na utekelezwaji wa mkataba wa Juba.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Audio Duration
2'37"
Photo Credit
UN Photo/Albert Gonzalez Farran