Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wagonjwa wengi wa Kisukari barani Afrika hata hawajitambui- WHO

Wagonjwa wengi wa Kisukari barani Afrika hata hawajitambui- WHO

Pakua

Wakati dunia ikiadhimisha hii leo siku ya kisukari duniani kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu ongezeko la mzigo wa ugonjwa huo na mikakati ya kuzuia na kudhibiti tishio lake, bara la Afrika linaonekana kuwa na changamoto kubwa ya ugonjwa huo, kwa mujibu wa takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO  Flora Nducha na taarifa zaidi

Takwimu zilizotolewa leo na WHO kanda ya Afrika zinaonyesha kiwango cha changamoto ya ugonjwa wa kisukari Afrika ni kubwa ambapo watu wazima milioni 24 hivi sasa wanaishi na ugonjwa wa kisukari na idadi inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 129 hadi kufikia watu million 55 ifikapo mwaka 2045. 

Kupitia ujumbe ake wa siku hii Dkt. Matshidiso Moeti mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amesema “Mwaka janga ugonjwa wa kisukari ulikatili maisha ya watu 416,000 barani Afrika na ugonjwa huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya vifo Afrika ifikapo mwaka 2030. La msingi zaidi ni kwamba kisukari ndio ugonjwaa pekee usio wa kuambukiza ambao hatari yake ya vifo vya mapema inaongezeka badala ya kupungua.” 

Mkuu huyo wa WHO Afrika ameendelea kusema kwamba “Sababu kuu hatari zinazochangia ongezeko la ugonjwa huo Afrika ni pamoja na  historia ya familia, ongezeko la umri na sababu zingine maarufu kama uzito wa kupindukia na utipwatipwa, maisha ya kukaa bila mazoezi, lishe isiyofaa, uvutaji wa sigara na unywaji pombe kupita kiasi. Kwa bahati mbaya, sababu hizi za hatari zinazoweza kubadilishwa zinaongezeka katika nchi zote katika Kanda ya Afrika ya WHO.” 

Dkt. Moeti amesema “Na changamoto kubwa katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo ni ukweli kwamba zaidi yam to 1 kati ya kila watu wawili barani Afrika anayeishi na kisukari hajawahi kupimwa  na hivyo kuongeza fursa za nyenzo za upimaji na dawa kama insulin,ni moja ya maeneo yanayopaswa kufanyiwa kazi haraka.” 

WHO imeonya kwamba ukiachwa bila kudhibitiwa, na bila usimamizi na mabadiliko ya mwenendo wa maisha, ugonjwa wa kisukari unaweza kusababisha matatizo mengine mengi.  

Matatizo hayo ni pamoja na mshtuko wa moyo, kiharusi, figo kushindwa kufanyakazi, kukatwa kwa viongo vya mwili kama miguu,  ulemavu wa kutoona, upofu, na uharibifu wa mishipa.  

Limeendelea kusema shirika hilo kuwa watu walio na ugonjwa wa kisukari pia wako katika hatari kubwa ya kupata dalili kali za COVID-19

Dkt. Moeti amesisitiza kuwa “Leo, tunapoadhimisha siku ya kisukari duniani, ninataka kuchukua fursa hii kutoa wito kwa serikali za nchi wanachama kuweka kipaumbele katika uwekezaji wa bidhaa muhimu, kama vile dawa za insulini, macshine za kuangalia kiwango cha sukaru glucometer na sindano zinazotumika kupimia au strips. Hii ni muhimu ili kuhakikisha fursa sawa kwa kila mtu anayeishi na ugonjwa wa kisukari, bila kujali ni wapi aliko katika bara hili.” 

Pia amezihimiza serikali za Afrika kupitisha na kubinafsisha malengo ya kimataifa ya ugonjwa wa kisukari, kama sehemu ya mapendekezo ya kuimarisha na kufuatilia hatua za ugonjwa wa kisukari ndani ya programu zao za kitaifa za NCD. 

Siku ya kisukari duniani huadhimishwa kila mwaka Novemba 14 na maudhui yam waka huu kama yalivyokuwa yam waka jana na yatakavyokuwa mwakani ni “Fursa ya huduma za kisukari” yakisisitiza umuhimu wa kuzuia na juhudi za hatua dhidi ya kisukari. 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Flora Nducha
Audio Duration
3'43"
Photo Credit
Eric Omondi, muuguzi wa Kituo cha Usimamizi na Taarifa za Kisukari anakagua eneo lenye uvimbe kwenye mkono wa Maingi.