Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutoe mguu kwenye kichochea mwendo kasi cha uharibifu wa mazingira- Katibu Mkuu UN

Tutoe mguu kwenye kichochea mwendo kasi cha uharibifu wa mazingira- Katibu Mkuu UN

Pakua

Mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP27 ukiingia siku ya pili hii leo huko Sharm el-Sheikh nchini Misri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewakumbusha viongozi wa dunia na wote wanaohudhuria mkutano huo kwamba suluhu ya changamoto ya mabadikio ya tabianchi iko mikononi mwao na wakati wa kuchukua hatua ni sasa kwani hakuna tena muda wa kusubiri. Flora Nducha na taarifa zaidi 

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha viongozi wa ngazi ya juu cha utekelezaji kwenye mkutano huo Antonio Guterres amesema katika siku chache zijao idadi ya watu duniani itafikia bilioni 8 idadi ambayo inainaupa maana zaidi mkutano huu wa COP27 hasa katika kuchukua hatua zinazohitajika kuepuka zahma ya mabadiliko ya tabianchi 

“Mkutano huu wa mabadiliko ya tabianchi ni kumbusho kwamba jawabu liko mikononi mwetu na saa zinayoyoma tuko katika vita vya kufa na kupona na tunashindwa vita hiyo, gesi ya viwanda inazidi kuongezeka, kiwango cha joto duniani kimefurutu ada na kinaendelea kuongezeka , dunia inaelekea mwisho ambao utafanya mgogoro wa tabianchi usiweze kurekebishwa. Tuko kwenye barabara kuu ya kuelekea kuzimu kwa mabadiliko ya tabianchi huku mguu wetu ukiwa bado kwenye kiongeza kasi.” 

Ameonya kwamba mabadiliko ya tabianchi yako kwenye ratiba tofauti, na kiwango tofauti na wa kulaumiwa ni sisi wenyewe  kwani shughuli za binadamu ndio chanzo kikuu cha janga la mabadiliko ya tabianchi, hivyo hatua za binadamu lazima ziwe suluhu, hatua za kujenga upya matamanio na hatua za kujenga imani hususani kati ya Kaskazini na Kusini. 

Amesisitiza kwamba sayansi iko bayana ili kuhakikisha nyuzi joto duniani inasalia nyuzi 1.5 ni lazima kufikia lengo la kukomesha kabisa uzalishaji hewa ukaa ifikapo 2050. 

Hata hivyo hivi sasa amesema lengo hilo liko kwenye njiapanda Na ili kuepuka hali hiyo mbaya, nchi zote za G20 lazima ziharakishe mabadiliko yao sasa katika muongo huu. Nchi zilizoendelea lazima zishike usukani na nchi mbili zenye uchumi mkubwa zaidi Marekani na Uchina zina wajibu mahususi wa kuunganisha juhudi ili kufanikisha lengo hili. Hili ndilo tumaini letu pekee la kufikia malengo yetu ya mabadiliko ya tabianchi. Ubinadamu una chaguo kushirikiana au kuangamia. Ni mshikamano kuhusu mabadiliko ya tabianchi au sote tuangamie.” 

 

Katibu Mkuu amesema athari za mabadiliko ya tabianchi tunazo sasa na hasara na uharibu zinazousababisha hauwezi tena kupuuzwa, kwa mantiki hiyo amesisitiza kwamba  “Katika kushughulikia hasara na uharibifu, mkutano huu wa COP27 lazima ukubaliane juu ya ramani ya mwelekeo ilio bayana, iliyo na wakati unaoakisi ukubwa na uharaka wa changamoto hii. Ramani hiyo lazima itoe mipango madhubuti ya kitaasisi ya ufadhili. Habari njema ni kwamba tunajua la kufanya na tuna nyenzo za kifedha na kiteknolojia ili kukamilisha kazi hiyo. Ni wakati wa mataifa kushikamana kwa ajili ya utekelezaji. Ni wakati wa mshikamano wa kimataifa kila kona.” 

 

Pia ametoa wito wa kuhakikisha duniani kote kunakuwa na mifumo ya tahadhari ya mapema ya majanga katika miaka mitano ijayo na serikali kuongerza kodi katika uzalishaji wa mafuta kisukuku kwani amesema jambo moja lililo wazi ni kwamba wale watakaokata tamaa watapoteza katika vita hivi na kupoteza vita hivi sio chaguo ni lazima kuvishinda. 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Flora Nducha
Audio Duration
3'15"
Photo Credit
© UNICEF/Sebastian Rich