Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushiriki mapema wa baba na mama kwenye malezi ya mtoto waongeza uelewa wa mtoto

Ushiriki mapema wa baba na mama kwenye malezi ya mtoto waongeza uelewa wa mtoto

Pakua

Nchini Zambia wakazi wa kijiij cha Kholowa wilaya ya Katete jimbo la Mashariki wameanza kuona manufaa ya mradi wa maendeleo ya mapema ya mtoto, ECD unaotekelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, mradi ambao alianza mwaka 2018 na unashirikisha baba na mama katika malezi ya mtoto tangu akiwa tumboni mwa mama yake hadi anapozaliwa na anapoendelea kukua. Taarifa ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi. 

Nyumbani kwa Posilio Phiri akisema UNICEF ilianza kwa kutufundisha jinsi ya kucheza na mtoto akiwa tumboni mwa mama yake. 

Video ya UNICEF inarejelea mwaka 2019 Posilio akiwa na mkewe mjamzito akishika tumbo la ujauzito huku wakizungumza kwa furaha. Na kisha video inasonga mbele kuonesha mtoto Moses ameshazaliwa na akiwa na afya njema ambapo Bwana Phiri anasema hata baada ya kuzaliwa tumeendelea kucheza naye. 

Mwaka 2020 mtoto Moses ameendelea kukua na anaonekana akicheza na mama yake na baba yake kwa kutumia vifaa vya michezo vya kutengeneza wao wenyewe ambapo Bwana Phiri anasema hakika huyu anajifunza mapema na haraka zaidi. 

Hoja yake inaungwa mkono na mkewe Sarah Nkoma akisema, ndugu zake walikuzwa bila malezi yoyote ya msingi. Naamini atakuwa na akili zaidi akianza shule kwa sababu ameanza kujifunza mambo mengi akiwa mdogo sana. Hii ni kwa sababu ya mambo mengi tunayomfundisha. 

Mwaka huu wa 2022 mtoto Moses amepiga hatua zaidi, ameshika mchoro wa ng’ombe anatazama, na kama haitoshi anacheza mpira na baba yake. 

Bwana Phiri kwa tabasamu anasema kinachonifurahisha na mtoto huyu ni kwamba ana akili sana na ni tofauti na marafiki zake. Tunafurahia sana mafunzo haya na tutayaendeleza. 

Kupitia mradi huu wa UNICEF ulioanza mwaka 2018, kwanza ilishirikisha wanakijiji umuhimu wa uwepo wa vituo  hivyo na kisha jamii ikatoa maeneo ya ardhi kwa ajili ya  ujenzi wake ambako hufundishwa umuhimu wa maendeleo  ya mapema ya mtoto. 

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta MAssoi
Audio Duration
2'6"
Photo Credit
© UNICEF/Kinny Siakachoma