Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

24 Mei 2022

24 Mei 2022

Pakua

Jaridani Jumanne, Mei 24, 2022 na Leah Mushi anaanza na

HABARI KWA UFUPI 

Nchi nyingi tajiri zinatengeneza hali isiyo ya afya, na ya hatari kwa watoto kote ulimwenguni, kwa mujibu wa ripoti mpya Ri iliyochapishwa leo na Ofisi ya Utafiti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.  Ripoti hiyo kwa jina Innocenti Report Card 17, ina viashiria kama vile kukabiliwa na vichafuzi hatari ikiwa ni pamoja na hewa yenye sumu, dawa za kuulia wadudu, unyevunyevu na madini ya risasi; upatikanaji wa mwanga, maeneo ya kijani na barabara salama; na michango ya nchi katika janga la tabianchi, matumizi ya rasilimali, na utupaji wa taka za kielektroniki. Ili kuonesha ukubwa wa tatizo, ripoti imesema, ikiwa kila mtu angetumia rasilimali kwa kiwango ambacho watu wa Canada, Luxemburg na Marekani hutumia, angalau ardhi dunia 5 zingehitajika ili kuendana na matumizi. 

=========================================== 

Mlipuko wa ugonjwa wa Monkeypox ambao umeripotiwa katika nchi 16 na kanda kadhaa za dunia, bado unaweza kuzuiwa, limesisitiza shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, WHO.  
"Tunachojua kutokana na virusi hivi na njia hizi za maambukizi, mlipuko huu bado unaweza kudhibitiwa; ni lengo la Shiŕika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO) na Nchi Wanachama kudhibiti mlipuko huu na kuukomesha.” amesema leo Dkt Rosamund Lewis, Mkuu wa timu ya kudhibiti ugonjwa wa ndui, ambayo ni sehemu ya Mpango wa Dharura wa WHO. Wataalamu wa WHO wanasema dalili za Monkeypox zinaweza kuwa sawa na zile zinazowapata wagonjwa wa ndui, na ingawa zinaweza kuonekana za kutisha kwenye ngozi lakini hazina hatari sana na mara nyingi ni vipele vinavyovimba na kuambatana na homa hali inayoweza kudumu kwa wiki mbili hadi nne. Zaidi kuhusu ugonjwa huu, tafadhali temelea wavuti wetu wa news.un.org/sw.  

==================================== 

Na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Uhamiaji (IOM) limetangaza kuwa limerejesha operesheni zake za kuokoa maisha kwa kuwarejesha kwa hiari wahamiaji wa Ethiopia kutoka Yemen.  Operesheni hii inalenga kuwasaidia wahamiaji wasiopungua 6,750 wanaoondoka katika nchi hiyo iliyoathiriwa na migogoro. Kufikia sasa, zaidi ya wahamiaji 600 wa Ethiopia ikiwa ni pamoja na watoto 60 wahamiaji wasio na walezi  wamewasili katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa wakitokea Aden, Yemen katika safari tatu za kwanza za ndege za wanaorejea kwa hiari. Safari za ndege za ziada zimepangwa kuondoka kutoka Yemen hadi Ethiopia katika wiki zijazo, lakini msaada mkubwa unahitajika haraka kusaidia wale wote wanaotaka kurejea, imeeleza taarifa ya IOM iliyotolewa hii leo mjini Aden na Addis Ababa. 

 

Katika mada kwa kina,kuelekea siku ya walinda amani tunaelekea nchini DRC kuzungumza na walinda amani

Na mashinani ni Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi aliyeko ziarani Bangladesh.

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
12'1"