Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

27 Aprili 2022

27 Aprili 2022

Pakua

Jaridani Aprili 27, 2022 na Leah Mushi kwanza ni habari kwa ufupi-

Takriban dola bilioni 1.4 zimeahidiwa na wafadhili kwa ajili ya kusaidia nchi zilizoko katika pembe ya Afrika zinazokabiliwa na ukame mkali kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 40. Ahadi hizo zimetolewa jijini Geneva, Uswisi katika mkutano wa ngazi za juu ulioandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya dharura -OCHA na Shirika la Muungano wa Ulaya la Ulinzi la Kiraia na Operesheni za Misaada ya Kibinadamu -ECHO, na kuhudhuriwa na wawakilishi wa serikali wa nchi zilizoathiriwa na ukame za Somalia, Kenya na Ethiopia. Ahadi hizo za fedha zitasaidia mashirika ya kibinadamu kutoa chakula cha dharura, lishe, fedha taslimu na usaidizi wa kiafya, pamoja na malisho na dawa ili kuweka mifugo hai. Tayari watu milioni 1 wameyakimbia makazi yao kutokana na ukosefu wa maji au malisho, na mifugo isiyopungua milioni 3 imekufa.  

===================================== 

Leo Aprili  27, Uingereza imetarifu Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO kuhusu kundi la wagonjwa wenye maambukizi ya Salmonella Typhimurium. Uchunguzi ulihusisha mlipuko huo na chokoleti inayotengenezwa nchini Ubelgiji, ambayo imesambazwa kwa angalau nchi 113. Tahadhari ya kimataifa ilitolewa na INFOSAN tarehe 10 Aprili, na kuanzisha mkakati wa kimataifa wa kurejeshwa kwa bidhaa. Kufikia sasa, jumla ya wagonjwa 151 wanaohusishwa na genetiki zinazoshukiwa kuhusishwa na ulaji wa bidhaa za chokoleti husika wameripotiwa  kutoka nchi 11. Hatari ya kuenea katika kanda ya Ulaya ya WHO na kimataifa inatathminiwa kuwa ya wastani hadi taarifa zipatikane juu ya urejeshaji kamili wa bidhaa hizo. 

 
=============================

Na Binti mfalme Basma bint Ali wa Jordan leo ameteuliwa kuwa balozi mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na kilimo, FAO kwa Mashariki ya Karibu na Kaskazini mwa Afrika. 

Katika jukumu lake jipya Binti mfalme atasaidia FAO kuongeza ufahamu kuhusu umuhimu wa kubadilisha mifumo ya kilimo cha chakula duniani, ili kuondokana na changamoto za kuendelea na kukua kwa njaa. 
Mkurugenzi Mkuu wa FAO QU Dongyu amesema kuwa Binti Mfalme amekuwa muungaji mkono wa muda mrefu wa FAO na mtetezi na mjuzi wa uhifadhi wa bayoanuai duniani kote na kusema, "Ufalme wake umeongeza ufahamu kwa watu wa Jordan na watu wote wa Mashariki ya Karibu. na Afrika Kaskazini  kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mimea asilia na mifumo ikolojia na kukuza utafiti wa bayoanuai na ujifunzaji wa mazingira, ambayo ni msingi wa kuhakikisha mifumo endelevu ya chakula cha kilimo na kuboresha uhakika wa chakula. 

Katika mada kwa kina  tutapata ujumbe kutoka kwa washiriki kutoka Burundi kwenye mkutano wa jukwaa la kudumu la watu wa asili ulioanza wiki hii.

Na katika mashinani ni ujumbe wa rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu ufunguzi wa jukwaa la kudumu la watu wa asili.

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
13'57"