Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa tutoke kwenye maneno na ahadi, twende kwenye kufanya kweli kuhusu mabadiliko ya tabianchi: Rais Samia

Sasa tutoke kwenye maneno na ahadi, twende kwenye kufanya kweli kuhusu mabadiliko ya tabianchi: Rais Samia

Pakua

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameelezea kile ambacho taifa lake na nchi nyingine zinazoendelea wanataka kuona kinatekelezwa baada ya mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP26 unaofanyika huko Glasgow Scotland.

Amesema hayo punde baada ya kuhutubia mjadala wa wazi wa mkutano huo unaofanyika wakati nchi tajiri zikisuasua kutekeleza ahadi zao akiongeza kuwa

"kwenye mkutano huu mengi yamezungumzwa lakini tunayopenda kusikia na tunayosukuma yazungumzwe ni sasa tutoke kwenye maneno na ahadi, twende kwenye kufanya kweli kwa sababu kila tunapokaa haya mabadiliko ya tabianchi yanaleta madhara mengi na tunavyoendelea kubishana  tutoe fedha au tusitoe madhara yanaendelea. Kwa hiyo nchi nyingi tumekubaliana nchi zilizoendelea ziache kuvuta ahadi zao na badala yake zitoe hizo fedha haraka ili nchi zinazoendelea ziendelee kutekeleza mipango tuliyojipangia ya marekebisho ya tabianchi.

Mara baada ya mkutano huo Rais Samia ameshiriki mkutano maalum wa wanawake viongozi ulioitishwa na kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon ukimulika nafasi ya viongozi hao katika kukabili mabadiliko ya tabianchi.

“Sisi wanawake viongozi wanawake tutaendelea kupaza sauti kwa ajili ya wanawake wenzetu, tutaendelea kuwataka viongozi wa dunia kuchukua hatua zaidi kutatua changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, tunataka kuona ahadi thabiti za kupunguza kiwango cha joto hadi nyuzi joto 1.5. Tusipofanya hivyo madhara ni makubwa zaidi kwa wanawake na watoto wa kike.”

Rais Samia ameelezea jinsi Tanzania ina mkakati maalum wa kitaifa wa kijinsia na mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2013 ambao lengo lake ni kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Baada ya mkutano huo viongozi hao wamesaini  tamko la pamoja la kupaza sauti katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'32"
Photo Credit
State House Tanzania