Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ng'ombe mmoja huko Burundi akomboa familia iliyokuwa taabani

Ng'ombe mmoja huko Burundi akomboa familia iliyokuwa taabani

Pakua

Mtamba mmoja wa ng’ombe anaweza kuonekana si chochote kitu kwa wafugaji wabobezi lakini kwa Beatrice Nibogora na familia yake nchini Burundi, mtamba huyo akipatiwa jina Maza amegeuka lulu na ufunguo wa maisha yenye matumaini na kutimiza methali ya wahenga ya kwamba baadhi ya dhiki ni faraja.

Hii ni baada ya mradi wa Benki ya Dunia na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kubisha hodi kunusuru kaya maskini. Anold Kayanda anafafanua zaidi.

(Taarifa ya Anold Kayanda)

Kutana na Beatrice Nibogora.. mama huyu anaishi na familia yake ambayo ni mumewe Sylvestre na mwanae Chanique kwenye umri wa miaka 3, katika vilima vya Rwimbogo nchini Burundi.

Kutana pia na Maza! Maza siyo tu kwamba ni mtamba mzuri wa kupendeza, usidanganyike! Maza ni mtamba ambaye amebadilisha maisha ya familia hii.

Kabla ya ujio wa Maza, Beatrice maisha yalikuwa ya tabu. Licha ya kilimo shambani, mlo wao ulikuwa ni mmoja kwa siku.

Siku moja, mradi wa Merankabandi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF nchini Burundi, ukabisha hodi nyumbani kwake kumuokoa yeye na familia  yake.

Katika kipindi cha miaka mitatu, mradi umepatia kaya maskini 56,000 ikiwemo ya Beatrice migao 15 ya dola 20 sawa na jumla ya dola 300, pamoja na mafunzo ya malezi ya watoto, afya ya mama na mtoto na usimamizi wa fedha,

Kupitia simu yake ya kiganjani, Beatrice alipokea fedha hizo za kujikimu. Kwa kiasi hicho kidogo cha fedha, alinunua nguruwe na kuku huku akidunduliza fedha.

Siku moja, alifanikiwa kumnunua Maza. Maza akazaa ndama na akaanza kuwapatia  lita 2 na nusu za maziwa kila siku. Beatrice pamoja na kumpatia mwanae Chanique maziwa ya kunywa, pia anatengeneza jibini.

Samadi kutoka kwa Maza ikawa mbolea shambani na rutuba ikaongezeka sambamba na mavuno.

Njaa imetoweka kwenye familia hii, na ameweza pia kuajiri kijana Jean-Marie anayemsaidia kukata majani ya ng’ombe.

Maza amegeuza maisha kuwa rahisi na shuku za awali zimetoweka na nuru imeonekana.

Audio Credit
Assumpta Massoi / Anold Kayanda
Sauti
1'58"
Photo Credit
UNICEFBurundi/2021/Ruben Hamburger