WFP yaomba msaada zaidi kusaidia nchini Ethiopia

WFP yaomba msaada zaidi kusaidia nchini Ethiopia

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limesema linashughulikia mara moja mahitaji yanayoongezeka na kuongeza msaada wa chakula cha dharura katika maeneo ya Afar na Amhara nchini Ethiopia. 
(Taarifa ya Jason Nyakundi) 

WFP inasema mizozo inazidi kuongezeka katika mikoa ya Afar na Amhara na hivyo hadi kufikia watu milioni saba wanahitaji msaada mkubwa wa chakula kaskazini mwa Ethiopia. 

Shirika hilo la mpango wa chakula duniani kwa kushirikiana na maafisa wa Serikali ya shirikisho Ethiopia pamoja na mamlaka ya Afar wanatoa msaada wa dharura wa chakula kwa zaidi ya watu 530,000 huko Afar.

Sadia, mama aliyefurushwa ka katika makazi yake na sasa anaishi katika hema dogo na watoto wake anaeleza alivyofika hapa kwa tabu,  “Oh, safari nzima ilikuwa kupitia jua kali na kiu ya kunywa maji ilikuwa ya uchungu sana. Tulilazimika kunywa maji ya mvua kwenye ardhi, ambayo pia yalitufanya tuwe wagonjwa. ” 

Kama ilivyo kwa Afar, Amhara nako hali ni hivyo. WFP inawasaidia takribani watu 200,000 waliofurushwa na takribani watu milioni moja wanahitajoi msaada wa haraka hasa wa chakula. 

Msafara wa WFP wa malori zaidi ya 100 uliingia Tigray juzi Jumapili ukibeba tani 3,500 za chakula na mizigo mingine ya kuokoa maisha ikiwa ni pamoja na mafuta, vifaa tiba na vitu vya makazi kwa niaba ya jumuiya ya misaada ya kibinadamu.  

Lakini hili ni tone tu baharini kama anavyoeleza Satyen Tait afisa wa WFP Ethiopia, "Hatuna akiba ya chakula kwa sasa kupanga au kusambaza. Chochote tulicho nacho kwa sasa kinasambazwa au tayari kimesambazwa. Kwa hivyo, kile tunachotazamia kwenda mbele ni hali ngumu kwetu kuendelea kutoa huduma kwa jamii zetu hapa. " 

WFP inasema uhakika wa chakula kwa mamilioni ya watu kote Ethiopia uko katika hatari kutokana na pengo la kifedha ambalo halijawahi kutokea kwa shughuli za WFP nchini humo. Kwa msingi huo WFP inatoa wito kuwa inahitaji dola milioni 140 kupanua huduma zake katika eneo la kaskazini mwa Ethiopia na dola za kimarekani 426 ili kutoa msaada kwa watu milioni 12 kote Ethiopia.  
 

Audio Credit
Grace Kaneiya / Jason Nyakundi
Audio Duration
2'23"
Photo Credit
© WFP/Claire Nevill