Skip to main content

Benki ya dunia yakarabati barabara nchini Afghanistan

Benki ya dunia yakarabati barabara nchini Afghanistan

Pakua

Maelfu ya wakazi wa Khushal Khan ambayo ni moja ya viunga vya jiji la Kabul nchini Afghanstan wanafurahia hali bora ya hewa na mitaa misafi baada ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa ukarabati wa barabara na mitaa  unaosimamiwa na Benki ya Dunia kwa niaba ya wafadhili wengine 34. 

(Taarifa ya Lucy Igogo) 
Ufadhili huo wa Benki ya Dunia kwa kushirikiana na wafadhili wengine na pia kwa usimamizi wa Manispaa ya Kabul, umeboresha jumla ya mitaa 33 kwa kuweka vitofali katika maeneo ya watembea kwa miguu, barabara za zege na lami na hivyo kuwanufaisha zaidi ya wakazi 7,000 wa Khusal Khan.

Mitaro, makaravati na njia za watembea kwa miguu vimejengwa ili kushughulikia tatizo la majitaka na pia usalama wa watembea kwa miguu. 
Azizullah Noori ni Mhandisi katika Programu ya Maendeleo ya Manispaa ya Kabul anasema, “tulipotembelea eneo, tuliona kulikuwa na umuhimu mkubwa wa mitaro. Karibia asilimia 90 ya mitaa haikuwa na lami. Ilikuwa inaweka ugumu kwa watoto  na kila mtu kutembea. Matope na madimbwi ambayo yalijaza mitaa yalifanya maisha ya watu kuwa mabaya.” 

Wakazi wa mitaa hii wanasema kwamba uchafuzi wa hewa umepungua na usafi kwa ujumla umeboreshwa kutokana na uwepo wa barabara zenye lami hali ambayo imeboresha pia afya zao. Mohammad Jamil Hamkar ni mkazi wa Khushal Khan anasema,  
(Sauti ya Mohammad Jamil Hamkar) 

“Zamani tulikuwa na shida nyingi sana. Mitaa ilikuwa mibaya sana, kulikuwa na vumbi kila mahali na tuliathirika na usafi duni kwa kuwa mazingira yetu yalijaa uchafuzi. Baada ya mitaa yetu kuwekewa lami, mambo yakawa mazuri. Ni mitaa yenye ubora mzuri na watu wanaifurahia. Mitaa sasa ni mizuri na imemnufaisha kila mtu.”

Mkazi mwingine ambaye anafurahia mradi huu ni Haji Mohammad Zahir ambaye pia ni Mwakilishi wa Jamii katika mradi huu, yeye anasema , “tulikuwa na matatizo mengi katika eneo letu. Hatukuwa na siku ambayo tungerudi nyumbani salama bila kuchafuka. Katika siku za mvua, mitaa ilikuwa inajaa matope  na siku za jua, vumbi linatapakaa kila mahali. Kuna chekechea hapa tulipo sasa hivi. Watoto walikuwa wanavuta vumbi ambalo lilikuwa linawafanya kuumwa. Tunamshukuru Mungu tumeondokana na matatizo hayo. Karibu hakuna mtoto katika maeneo haya ambaye amekuwa na kikohozi kwa mwaka sasa. Zamani vikohozi vilikuwa kawaida hapa.” 
 

Audio Credit
Assumpta Massoi / Lucy Igogo
Audio Duration
2'22"
Photo Credit
World Bank/Ghullam Abbas Farzami