Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa fedha kwa wakimbizi wawajengea uwezo wa kujitegemea

Msaada wa fedha kwa wakimbizi wawajengea uwezo wa kujitegemea

Pakua

Uganda nchi inayoongoza kuhifadhi wakimbizi wengi zaidi barani Afrika, imeshuhudia kuongezeka kwa mahusiano mema baina ya wakimbizi na wananchi waliowakaribisha baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula WFP, kuanza kutoa msaada wa kifedha kwa wakimbizi hali inayowawezesha wakimbizi kununua bidhaa kutoka kwa wanajamii pamoja na wao wenyewe kufungua biashara zao. 
 
(Taarifa ya Leah Mushi ) 
 Uganda inahifadhi zaidi ya wakimbizi milioni 1 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo – DRC, Burundi na Sudan Kusini. 
 Awali wakimbizi walipokea kutoka WFP misaada muhimu lakini ujio wa ugonjwa wa Corona au COVID-19 ulisababisha mgao kuwa wa fedha. 
 Katika video ya WFP wakimbizi wako kwenye foleni wakipata mgao wa fedha kutoka gari la huduma za kibenki, fedha kwa ajili ya kujikimu. 
 Kutokana na kusambaa kwa janga la COVID-19 nchini Uganda, msaada nao umeongezeka katika maeneo 9. Judith Agaba, Afisa wa WFP mjini Mbarara anasema katika ukanda wa kusini mashariki, asilimia 90 ya msaada unaotolewa kwa sasa ni fedha taslimu. 
 “Kama WFP hatujaamua tu kutoa msaada wa fedha kwasababu ya janga la Corona, kulikuwa na sababu nyingine zinazohusisha kuendeleza uchumi wa wanajamii katika wilaya zilizo wapokea wakimbizi” 
 
Mgao huu wa fedha umesababisha WFP kubaini uhaba wa miundombinu ya kibenki hivyo wanatumia wakala wa benki na kwingine magari yenye kutoa huduma za kibenki yanafika karibu na kambi. 
“Kwa sababu za kiusalama, tumekuwa tukileta mawakala hawa watugawa fesha karibu kabisa na makambi ya wakimbizi  ili wakimbizi wasiende mbali na makazi yao kwa ajili ya kupokea msaada huu wa fedha. kwa mfumo mwingine wa Card, wakimbizi wanaweza kutumia card kununua chakula madukani kama ambavyo watu wengine wanaweza kufanya hivyo kwakutumia Mastercard kwenye maduka makubwa” anasema Judith 
 
Gumisiriza Aloysius, msimamizi wa wakimbizi wilaya ya Isingoro anasema fedha hizi zimeongeza upendo katika jamii 

 “Kuwapatia fedha wakimbizi kunasaidia kuinua uchumi wa wilaya walizopo wakimbizi sababu sasa kuna kubadilishana biashara kati ya wananchi na wakimbizi. Wananchi wetu wanafanya kazi kwa bidi na wana mazao lakini walikuwa na changamoto ya soko, lakini sasa wanauhakika wa soko sababu wakimbizi wanahela. Halafu pia itaimarisha utulivu zaidi, kwasababu kwakweli utaachaje kumpenda na kumuheshimu mteja wako? Kwahiyo kwasasa kuna utulivu na uhusiano mwema kati ya wazawa na wakimbizi.”  
 
Wakimbizi nao wanasemaje kuhusu msaada huu wa kifedha kutoka WFP? Murebwayire Gativa ni mkimbizi ambaye sasa amefungua biashara ya ushonaji, 
 “Fedha taslimu ninazopokea kama msaada wangu wa chakula, natumia kiasi kununulia chakula, na kiasi kinachobaki, nakiongeza kwenye biashara yangu”  
 
Kwa kutambua kuna wakimbizi waliotoka nchi ambazo hawakupata kabisa elimu ya matumizi sahihi ya fedha, WFP imeanzisha mafunzo ya matumizi sahihi ya fedha ambapo familia, au baba na mama wanahudhuria pamoja mafunzo hayo. 
 
Murebwayire akiwa pamoja na wakufunzi, wanapanga bajeti akiwa katika eneo lake la biashara ya ushonaji, na  anasema  
“Hapa kama wakimbizi tumewezeshwa kupata mafunzo haya mazuri sana ambayo yametusaidia kubadili fikra zetu. Nashukuru sana mafunzo haya yametufungua akili zetu, sasa tuna uelewa wa kuweka akiba.”  
 
Msaada huu wa fedha unatolewa kila baada ya miezi miwili ili kupunguza changamoto mbalimbali ikiwemo kuwaweka hatarini wakimbizi wanapopokea fedha na kuwasaidia wale wanaojifunza kuweka akiba. 
 
Msaada huu wa fedha pamoja na kupanua masoko unawasaidia wakimbizi kuwa thabiti zaidi, kuziwezesha jamii, lakini pia kuwatoa wakimbizi kutoka kuwa wategemezi mpaka kuwa na uwezo wa kujitegemea wenyewe. 
  
 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Audio Duration
4'4"
Photo Credit
© UNHCR/Rocco Nuri