Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sanaa inayoifanya inanikumbusha nyumbani na kunipa matumaini: Mkimbizi Akram

Sanaa inayoifanya inanikumbusha nyumbani na kunipa matumaini: Mkimbizi Akram

Pakua

Msanii mkimbizi Akram Safvan kutoka Syria hadithi yake ni ya machungu, uvumilivu na matumaini. Baada ya vita kuzuka nchini mwake aliacha kila kitu na kukimbilia Uturuki na familia yake ambako sasa amejenga maisha mapya na kuponya machungu ya vita kupitia kazi ya sanaa ya uchongaji. Flora Nducha anasimulia zaidi 

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA) 

Natss….. 

Mjini Sanliurfa Uturuki msanii Akram yuko katika harakati zake za uchongaji na ni miongoni mwa mamilioni ya wakimbizi walio chini ya ulinzi maalum wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR nchini Uturuki. 

Alianza kazi ya Sanaa tangu angali mtoto nyumbani Syria akichora na baadaye kuchonga na aliwahi kushinda mashindano mbalimbali shuleni na hata kufungua studio yake ya kazi za sanaa akiwa na umri wa miaka 10 tu. 

Wakati huo kazi zake zilimulika mambo mbalimbali  yaliyoleta faraja na furaha lakini sio sasa ambapo anasema fikra zake zimebadilika 

(SAUTI YA AKRAM 1- KAMAU) 

“"Ninajaribu kuonyesha maumivu yangu, na maumivu ya jamii yangu huko Syria na, kwa jumla, kuonyesha mateso ya ulimwengu kupitia vita." 

Akiwa nyumbani Syria tayari alikuwa msanii mwenye jina lakini mambo yalibadilika na pia maisha aliyoyajua vita vilipozuka miaka 10 iliyopita. Kwanza alitaka kusalia Syria ili asiache kazi zake za sanaa na mapambano yaliyoshika kasi 2016 hakuwa na jinsi bali kufungasha virago na kuukimbia mji wa Deir Ezzor na kwenda kusaka hifadhi uturuki, mwaka mmoja baadaye familia yake na wanawawe watatu wakamfuata, anasema sanaa iko damuni mwakwe kwani 

(SAUTI YA AKRAM 2-KAMAU) 

“Nilizaliwa katika familia ya wasanii, familia yenye washairi, wasimulizi wa hadithi na waigizaji, na kwa miaka 30 nilikuwa nachora na kisha nimeanza kuchonga. Nchini Uturuki nina fursa ya kujieleza kwa sababu ya kile kinachoendelea Syria, siwezi kurejea huko”. 

Kazi ya sanaa Uturuki inamsaidia Akram kuishi yeye na familia yake na alipata fursa ya kuonyesha sanaa yake mara nne kwenye maonesho mbalimbali. 

Alipoondoka Syria Akran alichimbia ardhini baadhi ya kazi zake za sanaa ili zisichukuliwe, alichosaliwa nancho sasa ni matumaini kwamba labda ipo siku mzozo utaisha ili arejee nyumbani. 

Uturuki ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani , milioni 3.6 kati yao wanatoka Syria na karibu 330,000 ni wakimbizi na waomba hifadhi kutoka nchi nyingine. 

Audio Credit
UN News/Flora Nducha
Audio Duration
2'34"
Photo Credit
Jorge Mario Álvarez Arango