Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani kutoka Uingereza walioko nchni Mali wapiga doria ya siku 28 Gao

Walinda amani kutoka Uingereza walioko nchni Mali wapiga doria ya siku 28 Gao

Pakua

Nchini Mali, kikosi maalum cha Uingereza kinachohudumu katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA kimeendesha doria ya siku 28 kutoka mji wa Gao hadi Tassiga jimboni Gao kwa lengo la kulinda raia, katika eneo hilo ambalo limekuwa likishuhudia matukio ya ukosefu wa usalama.

Kwenye mji wa Gao jimboni Gao, kusini-mashariki mwa Mali, walinda amani kutoka Uingereza wanaohudumu katika kikosi maalum cha MINUSMA wakijiandaa kuanza doria ya siku 28 kutoka mji wa Gao hadi Tassiga. 

Eneo hili limekuwa linakumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa watu waliojihami na kusababisha majeruhi na vifo siyo tu miongoni mwa raia bali pia walinda amani. 

Meja Jamie Powell, ni kamanda wa kikosi cha Uingereza. “Kila tunapofika kijijini, watu wanahofia wakati mwingine kuzungumza nasi na kutupatia taarifa. Ni dhahiri hatutaki kumweka mtu yeyote hatarini, lakini tunasaka taarifa ili tuweze kuwasaidia kiusalama.” 

Ili kulinda kijiji hiki dhidi ya mashambulizi ya visasi kutoka kwa magaidi, Meja Powell na kikosi chake walikesha usiku mzima wakisubiri kikosi cha kukabili magaidi cha jeshi la Mali, FAMA, ambao waliendelea na lindo, huku waingereza wakiendelea na doria hadi Tassiga wakipitia mji wa Ansongo, umbali wa zaidi kilometa 1,200. 

Poppy Rogers, mlinda amani kutoka Uingereza akaelezea uzoefu wake kwenye doria hii.“Imekuwa ni uzoefu mzuri sana kutembelea vijiji mbalimbali na kukutana na watu wengi. Ni matumaini yetu kuwa uwepo wetu umekuwa na manufaa na kuhakikishia wananchi amani na kuzuia ugaidi. Nahamasisha wanawake wajiunge na kazi hii ya ulinzi wa amani.” 

Kwa jeshi la Mali, doria hii imekuwa na mchango mkubwa kwenye amani kama anavyosema Luteni Lancinet Camara. “Ushirikiano kati ya MINUSMA na FAMA kwenye sekta hii ni mzuri mno, hususan katika kubadilishana taarifa kati yetu. Tunatamani ushirikiano huu uendelee.” 

Audio Credit
Grace Kaneiya/Jason Nyakundi
Audio Duration
2'6"
Photo Credit
MINUSMA/Gema Cortes