Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: Tutumie siku ya afya duniani kuboresha mifumo ya afya

Guterres: Tutumie siku ya afya duniani kuboresha mifumo ya afya

Pakua

Kuelekea siku ya afya duniani kesho tarehe 7 mwezi Aprili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametilia mkazi maudhui ya mwaka huu ya siku hiyo ya afya ambayo ni kujenga dunia ya usawa zaidi na yenye haki, kwa kuzingatia jinsi janga la coronavirus">COVID-19 limefichua ukosefu wa usawa na haki kwenye mifumo ya afya. Taarifa ya Jason Nyakundi inaeleza zaidi. 

"Katika siku ya afya, tunaangazia ukosefu wa usawa na haki katika mifumo ya afya ambapo janga la Corona limeonesha jinsi jamii zetu zisivyo sawa! Ndivyo alivyoanza ujumbe wake Katibu Mkuu Guterres akisema hata ndani ya nchi, magonjwa na vifo kutokana na COVID-19 yamekumba zaidi watu na jamii zilizogubikwa na umaskini, mazingira magumu ya maisha na ya kazi, zinabaguliwa na zilizotengwa. 

Chanjo dhidi ya COVID-19 imepatikana lakini bado ni nchi tajiri zaidi ndio zimenufaika,  akisema jawabu ni huduma ya afya kwa wote.

 Nchini Afrika Kusini, taifa linaloongoza barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa COVID-19, Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la kuhudumia watoto UNICEF, linatumia gari lenye matangazo na simulizi za waathirika wa COVID-19 ili kupitisha ujumbe wa kujikinga. Mmoja wa wanufaika ni Brenda Khoza. 

 “Tuliathiriwa sana na hili janga, hasa familia yangu. Awamu ya kwanza nilipoteza watu wawili kwenye familia yangu, katika awamu hii ya pili wanafamilia watatu wamekufa. Jamii lazima isikilize serikali inaposema tunawe mikono na tusichangamane” 

Gari linatoa pia huduma za chanjo dhidi ya Corona na vipimo kama asemavyo dereva huyu wa teksi, Sthembiso Xulu. “Mpango huu umenisaidia sana kwa sababu muda mwingi tuko njiani na hatuna muda. Sasa nina fursa ya kuchunguza afya yangu. Wamegundua ni na shinikizo la damu linaloweza kuwa hatari kwa afya yangu, sasa nafahamu cha kufanya. Bila hili gari nisingalijua.” 

Wakati Guterres anataka kila mtu kuazimia kufanya kazi ili kuwa na dunia yenye uwiano na usawa na afya, mshauri wa mawasiliano wa UNICEF nchini Afrika Kusini Pumla Ntlabati anajinasibu na mradi wao akisema unalenga kuleta usawa kwa kuwa “ni moja ya mbinu zetu bunifu za kupeleka ujumbe kwa wananchi. Lengo zima ni kupeleka ujumbe pale ambako watu wapo. Gari hili linaweza kutangaza ujumbe kadri linavyotembea na unaona watu wanageuka kulitizama. Unaona watoto wanachukua hatua baada ya kuona ujumbe huo.” 

Audio Credit
Grace Kaneiya/Jason Nyakundi
Audio Duration
2'38"
Photo Credit
UNSOM