Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo kutoka UN yapatia watoto wa kike kujiamini

Mafunzo kutoka UN yapatia watoto wa kike kujiamini

Pakua

Nchini Tanzania, mradi unaotekelezwa na mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa, lile la sayansi, elimu na utamaduni, UNESCO, la masuala ya idadi ya UNFPA na la wanawake UN Women, umewanufaisha wasichana kuzitimiza ndoto zao kupitia kujifunza ujuzi na maarifa mapya. Fuatana na Ahimidiwe Olotu katika sehemu hii ya kwanza ya ripoti hiyo.

Kutana na Angel mwenye umri wa miaka 17 na Fatma mwenye umri wa miaka 24. Hawa ni miongoni mwa wanufaika wa mradi huu wa mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa. Katika darasa la sayansi, Angel alikuwa na tatizo la kutokujiamini. Kwa upande wa Fatma, yeye hakupata nafasi ya kumaliza elimu yake, alikwamia kidato cha nne. 

Walimu wa Angel wanasema hali yake ya kutokujiamini ilitoweka pale ambapo kupitia mradi huu wa UNESCOUNFPA na UN Women ulipowafikia. Angel mwenyewe anaeleza alichojifunza na hatua aliyoichukua, “Unatakiwa ujiamini kwamba sio wale wote wanaochukua sayansi ni wavulana tu. Pia hata msichana anaweza. Baada ya kupewa yale mafunzo, nilikaa nikajifikiria, nikaweka kiooo mbele yangu, nikajiambia, ‘Angel, hutakiwi kushindwa.’  Nilifanya vizuri mno na mpaka wakashangaa kwamba, msichana awamu hii kutuongozea Fizikia?! Hii yote ni kwasababu nilijiamini, nikajiambia kwa nini mimi nishindwe?” 

Kwa upande wa Fatma, amepata mafunzo ya kadhaa ya ufundi stadi, ujasiriamali, na hata kusoma na kuandika kulikokuwa kunamsumbua, hivi sasa si shida tena na hata anaweza kuwafundisha wenzake, “Kusoma naweza, lakini ni pale nilipojiunga na mpango huu, naweza kusoma sentensi. Tunajitahidi sana kuwafundisha wenzetu pale, kama mtu hajui kabisa kusoma, anaweza kusoma.” 

Fatma na Angel, wanaeleza faida za ujumla za mradi huu, kwanza ni Fatma, “Kusingekuwa na huu mradi, wasichana, tungelibaki wengine kuolewa, wengine kuzaa utotoni. Fikira zangu mimi ninataka nifungue duka, ili niweze kuwafunza wenzangu, niwe naweka vitu vyangu pale. 

Kisha Angel, “Huu mradi umesaidia kuinua vijana, kutetea haki za vijana, kuimarisha upendo kati ya watoto na wazazi wao.” 

Katika sehemu ya pili, tutawasikia walimu, wazazi na jamii walivyoupokea mradi huu wa kuwainua wasichana. 

 

 

Audio Credit
Flora Nducha/Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
2'50"
Photo Credit
© UNICEF/Jessica Jackel