Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajukuu zangU niliwakalisha kuwaambia, tazama, kuna njaa, sijui ni maisha gani tutaishi-Albertina

Wajukuu zangU niliwakalisha kuwaambia, tazama, kuna njaa, sijui ni maisha gani tutaishi-Albertina

Pakua

Zambia ni moja ya nchi tisa kusini mwa Afrika ambazo zinakumbwa na janga au viwango vya dharura ya ukosefu mkubwa wa uhakika wa chakula. Familia zinakabiliwa na hali mbaya kutokana na hali mbaya ya hewa kusababisha mavuno kuwa mabaya mwaka hadi mwaka na ni dhahiri hali ingekuwa mbaya zaidi kama si msaada kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau, ambao unaleta mabadiliko makubwa katika katika maisha ya kila siku ya watoto na familia zao. Assumpta Massoi na taarifa kwa kina.

Zaidi ya watu milioni 2.3 wameathiriwa na ukame mkali nchini Zambia, kati yao, watu 800,000 wakiwa katika Wilaya ya Gwembe kusini mwa nchi. 

Bibi mmoja aitwaye Albertina anaonekana akiwa amekaa kwenye kiti cha magurudumu, mbele ya nyumba yake. Ni mkulima mdogo kusini mwa Zambia anayetegemea mvua za msimu lakini ukame mkali umeharibu mazao yake kwa miaka mitatu mfululizo. Albertina katika mwonekano wa kukata tamaa anasema, “njaa ya mwaka huu ni kitu ambacho sijawahi kukiona katika maisha yangu yote. Ni vigumu pia kuomba chakula kutoka kwa marafiki siku hizi.” 

Wakati wa ukame, kuugua kumemfanya Albertina asiweze kutembea.  Kazi ndogondogo ambazo mabinti zake walikuwa wanazifanya, nazo zinaonekana kukauka.  

Mzani wa kupima uzito wa mtoto umetundikwa katika mti, muhudumu wa afya anampima mtoto. Mjukuu wa Albertina aitwaye Clinton, aligundulika kuwa na utapiamlo lakini bahati nzuri anapata matibabu kwenye kituo cha afya cha maeneo hayo kinachosaidiwa na UNICEF.  

Albertina pia yeye amepokea msaada wa dharura wa dola 40 kutoka ushirikiano wa UNICEF, seikali ya Zambia na wadau. 

Amezitumia fedha hizi kununua mbuzi, gunia la mahindi, chakula cha nyumbani na vitabu kwa ajili ya wajukuu wake.  

Mwaka huu mvua zimekuwepo lakini mavuno yake bado yanatishiwa na uvamizi wa viwavi jeshi. Bi Albertina anajishika paji la uso, anasema, “hii ni shida. Niliwakalisha wote chini na kuwaambia wajukuu zangu, tazama, kuna njaa, sijui ni maisha gani tutaishi.”  

Albertina na familia yake wanaishi kwa mashaka siku hadi siku. Kila janga, liwe la mazingira au jingine, lina athari mbaya kwa familia, hususani kwa wenye umri mdogo.  

 

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta Massoi
Audio Duration
2'15"
Photo Credit
© UNICEF/Karin Schermbrucker