Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN Women/UNDP: COVID-19 kuwatumbukiza wanawake wengine milioni 47 katika ufukara

UN Women/UNDP: COVID-19 kuwatumbukiza wanawake wengine milioni 47 katika ufukara

Pakua

 Takwimu hizo za pamoja zinasema kiwango cha umasikini kilitarajiwa kushuka kwa asilimia 2.7 kati ya mwaka 2019 na 2021 lakini makadirio sasa yanaonyesha kutakuwa na ongezeko la umasikini la asilimia 9.1 kutokana na athari za janga la corona au COVID-19.  Jason Nyakundi na taarifa zaidi. 

Makadirio hayo yanaonyesha kuwa janga la COVID-19 litaasababisha umasikini duniani kote, na wanawake ndio wataathirika zaidi hususani walio katika umri wa kuzaa. 

Na hivyo yamesema ifikapo mwaka 2021 kwa kila wanaume 100 wa umri wa kati ya miaka 25 na 34 wanaoishi katika umasikini uliokithiri au ufukara wa chini ya dola 2 kwa siku kutakuwa na wanawake 118, na pengo hilo linatarajiwa kuongezeka hadi wanawake 121 kwa kila wanaumee 100 ifikapo mwaka 2030. 

Hali halisi ya umasikini kwa wanawake 

Mkurugenzi mtendaji wa UN Women Phumzile Mlambo Ngcuka akizungumzia pengo hilo amesema “Ongezeko la wanawake kutumbukia katika ufukara hususan katika hatua hizo mbili za maisha yao ni ishara iliyo dhahiri ya mapungufu makubwa ya njia tulizoziweka za ujenzi wa jamii zetu na uchumi wetu. Tunajua kwamba wanawake ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa kuhudumia familia ,wanalipwa ujira kidogo, wanaweka akiba ndogo na wanafanyakazi zisizo na uhakika, ukweli ni kwamba kwa ujumla ajira ya wanawake iko hatarini kwa asilimia 19 zaidi ya wanaume.” 

Bi. Ngcuka amesisitiza kwamba Ushahidi uliopo wa mapengo ya usawa ni muhimu hatua zikachukuliwa na sera ambazo zitawaweka wanawake katika kitovu cha kujikwamua na janga hili. 

Takwimu hizo zilizoainishwa katika ripoti ya UN Women iliyopewa jina “Kutoka kwenye wazo kuingia kwenye hatua:Usawa wa kijinsia wakati wa COVID-9” zinaonyesha kwamba janga hili la COVID-19 litawatumbukiza watu milioni 96 kwenye ufukara ifikapo 2021, na milioni 47 kati yao ni wanawake na wasichana. 

Na takwimu hizo zitaongeza idadi ya wanawake na wasichana wanaoshi katika umasikini wa kupindukia hadi kufikia milioni 432, huku matarajio yakionyesha kwamba ifikapo mwaka 2030 idadi hiyo haitoshuka na kufika kiwango cha ilivyokuwa kabla  ya mlipuko wa janga la COVID-19. 

COVID-19 tishio kubwa katika kutokomeza umasikini 

Takwimu hizo mpya pia zinasema janga hilo ni tishio kubwa katika matarajio ya kutokomeza umasikini ifikapo mwisho wa muongo huu. 

Na huenda ukweli halisi ukawa mbaya zaidi  hasa ukizingatia kwamba haijajumuisha sababu nyingine kama vile wanawake kuacha kazi ili waangalie watoto wao wakati huu wa COVID-19 hali ambayo itaathiri mgawanyiko wa umasikini. 

Kwa upande wake mkuu wa UNDP Achim Steiner amesema “Wanawake na wasichana zaidi ya milioni 100 wanaweza kuinuliwa kutoka kwenye umasikini endapo serikali zitatekeleza mkakati wenye lengo la kuboresha fursa za elimu na uzazi wa mpango, haki na usawa katika ujira na kupanua wigo wa masuala ya kijamii. Wanawake wanabeba gharama za COVID-19 kwani wako hatarini zaidi kupoteza vyanzo vyao vya mapato na si rahisi kulindwa na hifdahi ya jamii hivyo kuwekeza katika kupunguza pengio la usawa wa kijinsia sio tu kwamba ni busara bali pia ni chaguo la haraka linaloweza kufanywa na serikali kubadili athari za janga la corona katika kupunguza umasikini.” 

Athari za COVID-19 ni zahma kila kona 

Ripoti hiyo ya UNDP na UN Women inasema athari za COVID-19 zitabadili mtazamo wa umasikini uliokithiri katika kila kanda.  

Wakati asilimia 59 ya wanawake masikini kabisa duniani hivi sasa wanaishi Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara, ukanda huo utaendelea kuwa mwenyeji wa idadi kubwa zaidi ya mafukara duniani. 

Na baada ya kupiga hatua kubwa katika kupunguza umasikini katika miaka michache iliyopita Asia Kusini inatarajiwa kukabiliana na kuibuka tena kwa umasikini uliokithiri. 

Ifikapo mwaka 2030 kwa kila wanaume 100 wa umri wa miaka 25 hadi 34 wanaoishi katika umasikini Asia Kusini kutakuwa na wanawake 129 masikini zaidi na hii itakuwa ni ongezeko kubwa kutoka makadirio ya 118 ifikapo mwaka 2021.  

Wakati takwimu hizi zinaogopesha utafiti unakadiria kwamba itahitaji asilimia 0.14 pekee ya pato la dunia sawa na dola trilioni 2 kuuinua ulimwengu kutoka katika umasikini uliokithiri ifikapo mwaka 2030, na dola bilioni 48 ndio zinazohitajika kuziba pengo la kijinsia la umasikini. 

Hata hivyo idadi kamili huenda ikawa ni ya juu zaidi endapo serikali zitashindwa kuchukua hatua au zitachelewa kuchukua hatua zinazohitajika. 

 

Audio Credit
Flora Nducha/Jason Nyakundi
Audio Duration
2'49"
Photo Credit
UNICEF/Shehzad Noorani