Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuondokewa na mwenza ni mtihani mkubwa lakini sikukata tamaa - Dkt. Jully

Kuondokewa na mwenza ni mtihani mkubwa lakini sikukata tamaa - Dkt. Jully

Pakua

Ikiwa leo ni siku ya wajane duniani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka kuangaziwa zaidi kwa kundi linalosahaulika mara kwa mara, wajane, hususan wakati huu wa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.  Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

Katika ujumbe wake siku ya wajane, Bwana Guterres amesema, “mwaka huu siku ya kimataifa ya wajane inafanyika wakati idadi ya vifo kutokana na COVID-19 inaendelea kuongezeka kila mahali hususan miongoni mwa wanaume. Hii ni fursa ya kipekee ya kuangazia kile ambacho husahaulika kila wakati kwenye majanga, yaani maisha na mustakabali wa wajane wanaobakia.”

Guterres amesema kifo cha mwenza katika wakati wowote ule huacha wanawake wengi bila haki ya kurithi mali na kwamba, “wakati wa janga la sasa, changamoto hizo huwa maradufu kwa wajane na huambatana na unyanyapaa na ubaguzi.”

Guterres amesema kadri harakati zozote za kujikwamua ziendane na mabadilko ya kimfumo ikiwemo kuondokana na sheria za kibaguzi kama zile za mirathi, suala ambalo linaungwa mkono na Dkt. Jully Goodluck, mjane huyu kutoka Tanzania ambaye anasema kuwa, “kuhusu suala la mirathi kusema ukweli, vyombo vya sheria vinavyohusika vinatakiwa vifanya kazi yao sawa sawa na kila mmoja awajibike kuhakikisha kwamba hao wajane hawahudhurii mahakamani kila siku, kwa sababu hao wenyewe wanatakiwa kutafuta kipato kwa familia zao. Kwa hiyo vyombo vya kisheria vinavyohusika vihakikishe kwamba hao wanawake wanapata haki zao kwa wakati.”

Na changamoto za maisha baada ya kuondokewa na mwenza ni zipi? Dkt. Jully anasema kwamba,""tangu mwanzo tulishazoea kushirikiana, tunafanya mambo kwa kushirikiana kwa hivyo kila mmoja alikuwa anamhitaji mwenzake  kwa namna moja au nyingine. Sasa unakuta baada ya kufiwa umebaki peke yako, huna mtu wa kukushauri, labda kuna kitu ulitaka msaada wa mawazo, hapo imekuwa ni changamoto kwa upande wangu, wakati mwingine unahisi upweke ya kwamba pengine angekuwepo mwenzangu ningeweza kufanya kitu fulani, unajikuta kwamba uko peke yako unafanya kila kitu peke yako na pengine hata kipato mlikuwa mnaleta pamoja, lakini umebaki kuwa wewe peke yako unayetegemewa. Hiyo ni changamoto kubwa sana.”

Tarehe 21 mwezi Desemba mwaka 2010, Umoja wa Mataifa kupitia azimio namba A/RES/65/189 la Baraza Kuu la Umoja huo, ulipitisha tarehe 23 mwezi Juni kila mwaka kuwa siku ya kimataifa ya wajane kwa lengo la kuangazia sauti na uzoefu wa wajane na kuchagiza msaada wa kipekee kwa kundi hilo.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'31"
Photo Credit
UN Photo.