Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yasema COVID-19 huenda ikawatumbukiza watoto wengine milioni 10 katika utapiamlo

WFP yasema COVID-19 huenda ikawatumbukiza watoto wengine milioni 10 katika utapiamlo

Pakua

Janga la virusi vya corona au COVID-19 huenda likawatumbukiza watoto wengine milioni 10 zaidi katika utapiamlo uliokithiri kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika la mpango wa chakula duniani WFP. Jason Nyakundi na taarifa zaidi

Katika kituo cha afya cha Koulaboi jimbo la Boke nchini Guinea kina mama na watoto wao wako katika foleni ya kutakasa mikono kisha kuingia kituoni kupokea msaada wa lishe kwa ajili ya kuwakinga watoto wao dhidi ya utapiamlo.

Makadirio ya WFP yanasema idadi ya watoto wanaougua utapiamlo uliotokana na lishe dunia inaweza kuongezeka kwa asilimia 20 kwa sababu ya mlipuko wa COVID-19.

Shirika hilo limeongeza kuwa hatua za kupambana na corona ikiwemo watu kusalia majumbani na kutotembea zimeathri sana maisha ya watu na kuongeza tishio lililokuwepo kama la vita na mifumo duni ya afya, na hivyo kufanya familia nyingi hasa katika nchi masikini kushindwa kumudu lishe bora. Lauren Landis ni mkurugenzi wa lishe wa WFP

COVID-19 na utapiamlo ni mchanganyiko hatari sana, virusi vinaweza kuwa na athari mbaya kwa miili ya watoto ambayo tayati iko dhaifu kutokana na lishe duni. Wakati huu wa janga tunaona familia nyingi zikihaha kuwapa watoto wao lishe bora kutokana na kupoteza kipato na kuathirika kwa masoko ya chakula, hii inaweza kusababisha mamilioni zaidi ya watoto kutumbukizwa katika utapiamlo na magonjwa.”

Sarah Nyak mwenye umri wa miaka 22 ni miongoni mwa watu hao kutoka familia duni hivi sasa yuko hospitali ya Sabah Juba, Sudan kusini amelazwa kwa sababu watoto wake wawii wako hoi na utapiamlo anasema

“Ikiwa watoto wangu wataishi nataka waende shuleni na wajifunze kujitunza wenyewe.”

Kote duniani watoto milioni 22 wa chini ya umri wa miaka mitano na kina mama wajawazito na wanaonyonyesha wanaitegemea WFP kuwapa lishe maalum kwa ajili ya kuzuia na kutibu utapiamlo.

Audio Credit
Jason Nyakundi
Audio Duration
2'3"
Photo Credit
Picha : WFP Burundi / Djaounsede Madjiangar