Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 haijali wewe ni nani, hivyo ni wakati wa kukomesha kauli za chuki duniani:UN

COVID-19 haijali wewe ni nani, hivyo ni wakati wa kukomesha kauli za chuki duniani:UN

Pakua

COVID-19 haijali sisi ni kina nani, tunaishi wapi, tunaamini nini au kuhusu tofauti nyingine yoyote. Tunahitaji kila aina ya mshikamano kulikabili janga linalotukabili la corona au COVID-19 kwa pamoja. Hayo yamesema na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Jason Nyakundi na taarufa zaidi 

Guterres ameyasema hayo katika ombi lake la kimataifa kushughulikia na kupambana na kauli za chuki wakati huu wa COVID-19. Ameongeza kuwa pamoja na jitihada lakini bado janga hili linaendelea kuzusha tsunami ya chuki na chuki dhidi ya wageni, ubebeshaji lawama na vitisho.

“Mtazamo wa kupinga wageni umeenea mtandaoni na mabarabarani. Nadharia za kupinga Uyahudi zimesambaa na mashambulizi yanayoambatana na COVID-19 dhidi ya Uislam yamefanyika. Wahamiaji na wakimbizi wametajwa kama chanzo cha virusi na kisha kunyimwa huduma za matibabu. Pamoja na wazee kuwa miongoni mwa walio hatarini zaidi dharau zimeibuka zikionyesha kuwa na wao pia ndio wanaokubwa zaidi. Na waandishi wa Habari, wanaodokeza ukweli, wataalam wa afya, wafanyakazi wa misaada na watetezi wa haki za binadamu wanalengwa kwa ajili tu ya kufanya kazi zao.

Katibu mkuu amesisitiza kwamba inapaswa kuchukua hatua sasa kuimarisha kinga ya jamii dhidi ya virusi vya chuki. Ndio maana anatoa ombi leo la juhudi za kila namna kukomesha kauli za chuki duniani. Na kwa wenye mamlaka Guterres amesema 

“Natoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuonyesha mshikamano na watu wote wa jamii zao na kujenga na kuimarisha mshikamano wa kijamii.

Natoa wito kwa taasisi za elimu kuzingatia ufundishaji wa kidijitali wakati ambao mabilioni ya vijana wako mtandaoni na wakati ambao wenye itikadi kali wanatafuta kuwinda mateka na hatimaye kurubuni watu hao.

Natoa wito kwa wanahabari na hususan makampuni ya mitandao ya kijamii kufanya juhudi zaidi kulingana na shheria za kimataifa za haki za binadamu, kuondoa ubaguzi wa rangi, mila potofu na na maudhui mengine mabaya.”

Pia amezitaka asasi za kiraia kuimarisha hatua za kuwafikia watu walio katika mazingira hatarishi na wadau wa kidini kutumika kama mifano ya kuheshimiana.

Amemtaka kila mtu kila mahali asimame dhidi ya chuki, kutendeana utu na kutumia kila fursa kuenzeza wema.

Amesema mwaka jana alizindua mkakati na mpango wa hatua wa Umoja wa Mataifa dhidi ya kauali za chuki ili kuimarisha juhudi za Umoja wa Mataifa dhidi ya jinamizi hili.

Amehitimisha kuwa “Tunapopambana na janga hili tuna wajibu wa kulinda watu , kutokomeza unyanyapaa na kuzuia machafuko. Hebu na tuzishinde kauli za chuki na janga la COVID-19 kwa pamoja.

 

Audio Duration
2'56"
Photo Credit
OCHA/Yaye Nabo Sène