Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Doria za pamoja za MINUSCA, CAR, zarejesha wakazi makwao

Doria za pamoja za MINUSCA, CAR, zarejesha wakazi makwao

Pakua

Walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya kati, CAR, MINUSCA wamefanya doria ya pamoja na vikosi vya jeshi la CAR huko ALindao, kusini mwa taif hilo kwa ajili ya kuhakikisha usalama kwa raia na waliofurushwa wakati ambako kunashuhudiwa shughuli za vikundi vilivyojihami. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

Hapa ni Alindao nchini, CAR ni maandalizi kabla ya safari ya doria kwenye maeneo ya raia. Walinda amani  wakiwa wamevalia mavazi yao ya kijeshi wamepiga mstari wakisikiliza maelekezo kutoka kwa kamanda wao, kisha wanakusanyika na kuingia kwenye vifaru ambavyo vinafuatana kimoja baada ya nyingine.

Meja Subodh Mohan Bhandari, ni mkuu wa kikosi cha walinda amani kutoka Nepal kwenye MINUSCA, kwenye eneo la Alindao.  

(Sauti ya Meja Subodh)

“Watu hapa wanajihisi wako salama zaidi kutokana na doria tunazozifanya kwa sababu tunazifanya usiku na mchana iwe ni doria ya miguu, au magari kwa hiyo watu wana furaha sana.”

Ili kuhakikisha usalama kwa raia, MINUSCA imeweka vituo vya ukaguzi katika maeneo maalum Alindao. 

Kapteni Asselet ni mkuu wa kikosi cha walinda amani kutoka Gabon kwenye MINUSCA.

(sauti ya Asselet)

« Tumeweka mikakati kuhakikisha kwamba jamii inahisi iko salama. Tulipanga kutoa ulinzi kwanza kisha kuweka mipango ya mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa mfano OCHA katika kiwango cha hospitali ya mkoa. Kisha tukazingatia usalama katika kituo cha wakimbizi wa ndani cha Elim. Tumeweka mzunguko wa duara 360 kati ya Elim, kituo chetu na barabara iliyopo nyuma yangu. »

Baada ya kurejea hali ya utulivu, sasa watu wameanza kurejea nyumbani kama anavyokiri Hamadou mkazi Alindao.

(Sauti ya Hamadou)

« Amani imeanza kurejea, na ndio maana tumerejea mjini na wake zetu na watoto. »

Kufikia mwisho wa mwezi uliopita wa Januari operesheni iliyopewa jina la "Mo Kiri" iliwezesha walinda amani wa MINUSCA pamoja na jeshi la taifa kusambaratisha vizuizi vilivyokuwa vimewekwa na kundi la watu waliojihami la UPC katika maeneo ya kuingia na kutoka jijini.

Audio Credit
UN News/Grace Kaneiya
Audio Duration
2'17"
Photo Credit
MINUSCA/Igor Rugwiza