Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfuko wa mazingira duniani na FAO wasaidia nchi kuwa na takwimu bora na sahihi za misitu

Mfuko wa mazingira duniani na FAO wasaidia nchi kuwa na takwimu bora na sahihi za misitu

Pakua

Shirika la Chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limezindua mradi mpya wenye thamani ya dola milioni 7.1 wa kuwezesha upatikanaji wa takwimu kuhusu misitu, takwimu zilizo za uwazi na haswa zinazosaidia nchi zinazoendelea kutekeleza makubaliano ya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi . Assumpta Massoi na ripoti kamili.

FAO inasema kuwa ufuatiliaji na utoaji taarifa kuhusu misitu na matumizi ya ardhi ni muhimu katika ufuatiliaji na utekelezwaji wa maendeleo endelevu.

Mradi huo unaofadhiliwa na GEF kwa dola milioni 1.9 na pia FAO ambayo inachangia dola milioni 5.2  ni moja kati ya miradi minne tu duniani iliyoidhinishwa na kufadhiliwa na mfuko  mpya unaosaidia nchi kutekeleza mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

 “Nchi nyingi zinazoendelea hukosa uwezo wa kutoa takwimu muhimu kuhusu misitu ili kuripoti mafanikio yao kuhusu tabianchi. Mradi huu utasaidia kuwepo mfumo wa kutegemewa na uwazi katika takwimu za misitu na kusaidia nchi kukusanya na kujumuisha data kuambatana na makubaliano ya Paris”, amesema Hiroto Mitsugi, naibu mkurugenzi wa FAO idara ya misitu.

Mradi huo utanufaisha moja kwa moja nchi 26 kote barani Asia, Afrika na Amerika Kusini na nchi zingine 185 kote duniani.

Utatekelezwa katika kipindi cha miaka miwili na idara ya msitu ya FAO ambayo tayari inasaidia nchi 70  kufuatilia misitu, kuhakikisha usimamizi bora wa misitu na utoaji wa ripoti za misitu zilizo bora.

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta Massoi
Audio Duration
1'23"
Photo Credit
UNMISS/Eric Kanalstein