Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana tunahitaji uhuru wa kutoa mawazo kuleta mabadiliko chanya- Wanjuhi

Vijana tunahitaji uhuru wa kutoa mawazo kuleta mabadiliko chanya- Wanjuhi

Pakua

Ikiwa kesho jumamosi vijana kutoka nchi mbalimbali wanachama wa Umoja wa Mataifa wanakutana jijini New York, Marekani katika jukwaa lao, Wanjuhi Njoroge, mwanaharakati kutoka Kenya ambaye atahutubia jukwaa hilo kubwa zaidi kuwahi kuandaliwa na Umoja wa Mataifa amesema kile ambacho atapaza katika ujumbe wake.

Akihojiwa na Idhaa na Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Bi. Njoroge amesema kuwa, “Nataka kuonyeshana ya  kwamba sisi kama watu ambao ni wachanga, wale watu ambao watakuwa kwenye jukwaa na wale ambao watakuwa wanatazama, tuna uwezo mkubwa sana. Ukiangalia kama Afrika tuko zaidi ya milioni 688 ama zaidi, tukija pamoja kama vijana tutaweza kufanya mambo mengi sana. La pili ni kusema ya kwamba tuliweza kufanya hili jambo Kenya kwa sababu tulipatiwa uhuru wa kufanya vile. Kenya haisemi kuwa huwezi kutumia mitandao ya kijamii kufanya hili ama lingine, sisi Kenya imetupatia nafasi ya kufanya hivyo, iko katika katiba yetu na pia Rais haji kusema kwamba hamuwezi kufanya vile. Wito mmoja wangu ni kwamba tupatieni uhuru sisi  vijana tuweze kufanya yale mambo ambayo tunapenda.”

Alipoulizwa ujumbe wake kwa vijana wa nchi zilizoendelea ambazo zinaongoza kwa uchafuzi wa mazingira huku Afrika ikibeba mzigo mkubwa wa madhara, mwanaharakati huyo kijana amesema, “tunawauliza vijana ambao watakuwa kwenye nchi ambazo zimeshaendelea, kwamba watie shinikizo kwa serikali zao ili wapunguze na watokomeze kabisa ule uchafuzi wa mazingira.”

Bi. Njoroge akaenda mbali zaidi kutoa mfano wa madhara ya uchafuzi wa mazingira akisema, “ukiangalia kama vitu vingi vinatoka Afrika, ukiangalia Ghana wanalima kokoa ambayo inatengeneza chokoleti. Sisi tunatoa maua, itaharibika, itakosekana , ile bidhaa itakosekana kwa kuwa wameharibu mazingira. Kwa hivyo hili jambo wanafanya watadhani itaathiri Afrika peke yake, lakini hapana hata wao watapata madhara kwa uharibifu wa mazingira.”

Audio Credit
Assumpta Massoi
Sauti
2'15"
Photo Credit
UN News Kiswahili/Jason Nyakundi