Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

"Back To Life" imebadili maisha ya waathirika wa madawa ya kulevya na kuwarejesha katika jamii- Masha Born

"Back To Life" imebadili maisha ya waathirika wa madawa ya kulevya na kuwarejesha katika jamii- Masha Born

Pakua

Hii leo ikiwa ni siku ya kupiga vita matumizi ya madawa ya kulevya duniani, vituo vya kusaidia waathirika wa madawa hayo vimekuwa msaada mkubwa wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa unasema ya kwamba watu milioni 35 ulimwenguni kote wana matatizo yatokanayo na matumizi ya madawa hayo ilhali ni mtu 1 tu kati ya 7 ndiye anayepata matibabu. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

Nchini Tanzania kituo cha Back To Life cha kusaidia waaathirika wa watumiaji wa madawa ya kulevya, kimekuwa msaada mkubwa kwa kundi hilo wakati huu ambapo ni mtu 1 tu kati ya 7 ya wanaotumia madawa ya kulevya ndio wanapatiwa matibabu.

Miongoni mwa wanufaika wa kituo hiki ni Masha Born mkazi wa Dar es salaam nchini Tanzania ambaye amekuwepo kituoni hapo kwa miaka 6.

“Nilikuwa nimeingia katika genge ambalo halikuwa sahihi katika maisha, halikuwa genge zuri, genge ambalo lilinitoa katika njia ya kutokuweza kuwepo karibu na marafiki, jamaa na ndugu,” anasema Marsha ambaye hivi sasa ni Meneja wa kituo cha Back To Life huko Kigamboni.

Masha akikumbuka hali aliyokuwa nayo zamani anasema kuwa, “unapokuwa katika utumiaji wa matakataka yetu haya ya madawa unatoka katika jamii, unajitenga kwa sababu wewe ulivyo hii leo si ambavyo ulikuwa huko nyuma.”

Kituo hiki kimemrejeshea utu akisema kuwa, “tuko na madarasa ambayo kuna sehemu tatu, asubuhi tunasoma kufahamu hisia zetu, kwa sababu hadi tumeingia kwenye lengo la kutumia, ni kwa sababu tulishindwa kumiliki hisia zetu. Mfano linakufika jambo zito, baba amefariki, na wewe unapata taarifa kupitia mtu mwingine ngoja  ule mshtuko, uoga na wasiwasi wa mabadiliko unaona bora nitafute kitu nibadilishe hisia, wewe unaona starehe kumbe si starehe.”

Back To Life kinawapatia stadi za kazi pia na hivyo anasema kwamba kwa miaka 6 aliyokuwepo kwenye kituo ameweza kupata misaada, watu wamerejea kwenye hali  ya kawaida, watu wameoa na kufanya shughuli zao kwa sababu nguvu kazi ya taifa ilikuwa inapotea barabarani.

Pili Missanah ni Mkurugenzi Mtendaji wa vituo vya Back to Life ambavyo kwa miaka 7 tangu kuanzishwa kwake vimeleta mabadiliko chanya kiasi kwamba hivi sasa, “serikali imeandaa muongozo kwa Sober Houses wa kuziongoza ili ziweze kufanya kazi katika kanuni na sheria zilizowekwa.”

Na Pili anatoa wito wake kwa jamii ni kwamba, “tusiwahukumu waathirika wa madawa ya kulevya, vituo vya kusaidia waathirika wa madawa ya kulevya vipo basi tuwapeleke waweze kupata huduma. »

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo, mwaka 2017 watu 585,000 walifariki dunia kwa matumizi ya madawa ya kulevya.

TAGS: Back To Life, Pili Missanah, Madawa ya Kulevya

Audio Credit
Arnold Kayanda/Assumpta Massoi
Audio Duration
2'7"duration
Photo Credit
UNIS