Wakimbizi ni watu kama sisi tusiwatenge- Mercy Masika

24 Juni 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR , limetea balozi mpya kutoka nchini Kenya, si mwingine bali ni muimbaji nyota wa nyimbo za injili na mwenye hamasa ya kusaidia jamii , Mercy Masika ambaye anasema atatumia kipaji chake kukirimu wakimbizi. John Kibego na maelezo zaidi.

Moja ya vibao mashuhuri vya nyota huyo kijulikanacho kama mwema. Ni rahisi kuona kwa nini Mercy Masika ambaye ni mshindi wa tuzo za nyimbo za injili anachukuliwa kuwa ni moja wa waimbaji wanopendwa sana nchini Kenya na hata nje ya mipaka ya nchi hiyo.

Mercy katika kipindi chote cha uimbaji wake ametumia sauti yake kuelezea upendo  kwa imani yake na jamii yake kupitia nyimbo mbalimbali kikiwemo kibao maarufu Nifunze

Mercy anasema upendo huo ndio uliomsukuma kuunga mkono kazi za UNHCR katika kuwalinda watu wanaolazimika kukimbia makwao kwa sababu ya vita, machafuko na mateso.”Imani yangu ya kikristo wakati wote imenifunza kuwaonyesha upendo wageni wanaotoka nje ya jamii yangu.”

Kwa takriban miaka miwili Mercy amekuwa akisaidia kampeni ya UNHCR inayotoa changamoto ya kuelewa kuhusu ukimbizi Afrika ijulikanayo kama UNHCR’s LuQuLuQu campaign. Kuhusu uteuzi wake Mercy anasema “ni heshima kubwa na furaha kupewa fursa hii. Wakimbizi ni watu kama wewe na mimi na wanaweza kuwa yeyoyote kati yetu, naamimi kama jamii ya Kiafrika tuna jukumu la kuonyesha utu wa kubebeana mizigo kwa kudhihirisha wema wetu kwa matatizo ya wakimbizi.”

Mercy amekuwa akitumia jukwaa lake la nyimbo kuelezea umuhimu wa kuwaonyesha huruma na upendo wakimbizi. Akipongeza kazi anayoifanya muimbaji huyo,  Fathiaa Abdala mwakilishi wa UNHCR Kenya amesema “Tunafurahi sana kwa Mercy kuteuliwa kuwa balozi mwema wa UNHCR nchini Kenya , nchi ambayo inahifadhi wakimbizi na waoomba hifadhi takribani 480,000. Kuwa na mtu mwenye kipaji, anayeheshimika na kuhamasisha wanawake kusaidia kuelimisha na kusaidia watu hawa ambao wamelazimika kukimbia ni thamani kubwa.”

Mercy Masikia alitangazwa rasmi kuvaa kofia hiyo ya balozi mwema  kambini Kakuma katika hafla maalumu ya siku ya wakimbizi duniani.

Audio Credit:
Assumpta Massoi/John Kibego
Audio Duration:
2'2"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud