Vijana changamoto zisiwakatishe tamaa bali ziwape chachu ya kusonga mbele- Isaya
Umoja wa Mataifa hivi sasa unataka vijana ndio wawe mstari wa mbele katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Ndio maana kila uchao kupitia mashirika yake mbalimbali chombo hicho chenye wanachama 193 kinapaza sauti kwa vijana kushiriki na kushirikishwa katika kila utekelezaji wa malengo hayo kuanzia kutokomeza umaskini, kusongesha amani, afya na hata ubia wa maendeleo. Tayari vijana wanaitikia wito na miongoni mwao ni Isaya Yunge, kijana mjasiriamali wa teknolojia kutoka Tanzania ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya Soma App na pia mwanzilishi mwenza wa kampuni ya teknolojia ya Smart Kaya au Nyumba Janja. Kampuni zao zimesonga na kubadili maisha ya wengi ikiwemo vijana huku akiwaacha watu wengi wakistaajabu na midomo wazi, lakini Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa alitaka kufahamu safari yake ilikuwa 'tamu tu' au iliambatana na shubiri? Na zaidi ya yote kulikoni yeye anajinasibu kama 'mtu mwenye matumaini asiyetikisika?'.