Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujangili wazidi kutishia uhai wa tembo Afrika

Ujangili wazidi kutishia uhai wa tembo Afrika

Pakua

Tathimini mpya iliyofanywa na ofisi ya mkataba wa kimataifa kuhusu biashara ya viumbe vilivyo hatarini CITES katika kitengo chake cha uafuatiliaji wa mauaji haramu ya tembo (MIKE) umethibitisha kwamba ujangili unaendelea kuwa tishio kubwa kwa mustakabali wa tembo barani Afrika. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

Kitengo hicho cha MIKE kimetoa tathimini hii kwa kuangalia idadi na kiwango cha mauaji haramu ya tembo na kugawanya na idadi ya mizoga ya tembo inayokutwa na askari wa wanyama pori wakiwa katika doria barani Afrika.

Kwa mujibu wa tathimini hiyo endapo “kiwango ni cha juu  zaidi ya 0.5 inamaanisha kwamba mauaji zaidi ya tembo yaliyoripotiwa yametokana na ujangili kuliko sababu zingine au vifo vya kawaida.

Na ushahidi uliokusanywa unaonyesha kwamba kiwango cha mauaji haramu ya tembo kiliongezeka mwaka 2011 na kufikia 0.77, wakati ambapo ujangili dhidi ya tembo wa Afrika ulikuwa asilimia 10. Kufikia mwaka 2017 kiwango kilishuka kidogo hadi 0.53 na kimesalia hapo hadi mwaka jana.

CITES imesisitiza kwamba kiwango kikubwa cha mauaji haramu ya tembo kinatia hofu “kwa sababu  hata katika maeneo ambayo yaweka ulinzi mzuri wa idadi ya tembo wao  vifo vya tembo vitokanavyo na ujangiri haviwezi kufidiwa na idadi ya tembo wanaozaliwa.”

Barani Afrika idadi ya tembo ni ndogo , wametawanyika na hawana ulinzi nzuri kwa mujibu wa tathimini na hivyo kuwafanya tembo katika bara hilo kuwa katika hatari kubwa dhidi ya vitendo vya ujangili.

Tathimini hiyo mpya ya CITES imesema ripoti ya hali ya tembo barani Afrika iliyotolewa mwaka 2016  inakadiria kwamba idadi ya tembo barani humo imepungua sana kutoka milioni 12 karne iliyopita hadi kufikia 400,000 hivi sasa.

Na imetoa wito kwa nchi, asasi za kiraia na wadau wengine wote wanaohusika na masuala ya Wanyama pori kuchukua hatua Madhubuti ili kuhakikisha tembo hao wanalindwa la sivyo wako katika hatari kubwa ya kutoweka.

Audio Credit
Arnold Kayanda/Assumpta Massoi
Sauti
1'47"
Photo Credit
UNEP GRID Arendal/Peter Prokosch